Breaking News

DK. MWANJELWA AITAKA TAKUKURU KUHAKIKISHA INADHIBITI MIANYA YA RUSHWA.


NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akizungumza na viongozi wa TAKUKURU nchini (hawapo pichani), wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa viongozi hao uliofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, Jijini Dodoma  jana.

 Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

SERIKALI imeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  kuelekeza nguvu zaidi kuhakikisha mianya ya rushwa ndani ya taasisi za umma na jamii kwa ujumla inadhibitiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutowaonea haya wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa bila kujali vyeo vyao.

  1. Hayo yamesemwa jana Desemba 13, 2018 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk . Mary Mwanjelwa  wakati akifunga mkutano mkuu wa siku mbili wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU nchini uliofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, jijini Dodoma.

Dk. Mary,  alisema watumishi wote wa TAKUKURU wamekula kiapo na wamepewa dhamana ya kuzuia na kupambana na rushwa, hivyo wametakiwa kutomuogopa mtu yeyote anayejihusisha na rushwa na kumshughulikia ipasavyo kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza  kuwa, katika kutekeleza azma ya serikali kufikia uchumi wa kati wa viwanda, TAKUKURU ikiwa ni taasisi iliyopewa dhamana na serikali ya kupambana na rushwa, haina budi kudhibiti vitendo vya rushwa katika sekta zilizopewa kipaumbele katika Mkakati wa Kitaifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Tatu (NACSAP III).

Naibu Waziri huyo  aliziainisha sekta zilizopewa kipaumbele, kuwa ni pamoja na sekta ya manunuzi ya umma, ukusanyaji wa mapato, maliasili na utalii, madini, gesi, afya, elimu na ardhi, hivyo TAKUKURU kuanzia ngazi ya wilaya inapaswa kutoa mchango kufikia uchumi wa kati wa viwanda.

Aidha,Mary alirejea maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu.  George Mkuchika kwa TAKUKURU alipokuwa akifungua mkutano huo ya kuwataka wadhibiti mianya ya rushwa katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani ambapo nae amesisitiza vitendo vya rushwa vidhibitiwe kikamilifu kwani ni kikwazo cha upatikanaji wa viongozi wenye sifa na uadilifu.Dk. Mary, akiwa na viongozi wakuu wa  TAKUKURU nchini kabla ya kufunga mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa viongozi hao uliofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, Jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi (CP) Diwani Athumani na kulia ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali. John Mbungo.

Dk .Mary  alisema  kuwa, suala la mapambano dhidi ya rushwa limepewa kipaumbele na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John  Magufuli, ambaye mara kwa mara amekuwa akionyesha hisia zake za dhati katika mapambano dhidi ya rushwa, hivyo TAKUKURU imuunge mkono kwa vitendo katika mapambano hayo.

Awali, akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi (CP) .Diwani Athumani amesema, katika kuboresha utendaji kazi na kufikia malengo ya taasisi yaliyokusudiwa, alitoa maelekezo kwa watumishi wote wa TAKUKURU kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili kuhakikisha uchunguzi unakamilika mapema iwezekanavyo na kuwafikisha watuhumiwa wa rushwa na ufisadi mahakamani.

CP. Athumani amesema, TAKUKURU inasimamia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Tatu (NACSAP III) ambao umeainisha jukumu la kila mdau katika kupambana na rushwa, hivyo ni jukumu la TAKUKURU kuhakikisha wadau wote wanauelewa na wanautekeleza kadri ilivyokusudiwa.VIONGOZI wa TAKUKURU nchini wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa viongozi hao uliofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa

Mkutano huo ulitoa fursa kwa viongozi wa TAKUKURU na wadau kujadili na kuweka mikakati madhubuti ya ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa.

No comments