Breaking News

HATIMAYE MADABIDA, KWIRASA, SANYA NA MADENGE WATOKA 'KIFUNGONI'.


 

WANACHAMA wanne waliosamehewa kufukuzwa uanachama wakiwa wamesimama mbele ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, akiwa na Makamu Mwenyekiti wake Philip Mangula na Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally na mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) (hawapo pichani), wakati wa  kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa leo Desemba 18, 2018 Jijini Dar es Salaam (Picha zote na Ikulu). 


 Na Thomas Mtinge

HATIMAYE kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kilichokaa leo Desemba 18, 2018 Jijini Dar es Salaam, kimetoa msahama kwa wanachama wake wanne waliokuwa wamefukuzwa uachama kutokana na makossa mbalimbali.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Bashiru Ally, ilisema kuwa wajumbe wa kikao kimepokea maombi na kukubali wanachama hao ambao walikuwa wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya, kurudishiwa uanachama.


SANYA na wenzake wakimshukuru Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, Makamu Mwenyekiti wake Philip Mangula na Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, waliosamehewa na kurudishiwa uanachama ni Ramadhani  Madabida, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Erasto Kwirasa, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Christopher Sanya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara na  Salum Madenge, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni.

Aidha, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kauli moja, iliamua kumuweka katika uangalizi mwachama Jesca Msambatavangu, ambaye aliomba kurejeshewa uanachama wa CCM baada ya kufukuzwa kwa makosa ya kimaadili.

Pia, Halmashauri Kuu ya CCM ilipitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama katika ngazi za wilaya, mkoa na taifa zilizoachwa wazi baada ya waliokuwa katika nafasi hizo kupangiwa majukumu mengine ya Kiserikali au  kufariki dunia pamoja na mgombea wa CCM wa kiti cha Ubunge katika Jimbo la Temeke Jijini Dar es Salaam.
     MADABIDA na wenzake wakiendelea kushukuru kwa viongozi wa meza kuu.

Taarifa hiyo iliwataja wanachama waliopitishwa na NEC kuwania nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kuwa ni Dk. Damas Mukasa Kashegu, Ashaha Juma Feruzi, Galila Ramadhani Wabanhu na Makene Pamella Boniphas.

Iliwataja pia wanatakaowania nafasi ya Uenyekiti wa CCM mkoani Iringa kuwa ni Dk. Abel Mwendawile, Aman Said Mwamwindi na Sabas Vitus Mushi, huku wanaowania nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi mkoa wa Simiyu ni Mashaka Abeid Makongoro, Mayunga Genga Ngokolo na Heri Mchunga Zebedayo.

Kwa upande wa watakaowania nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Mwanza ni pamoja na Bahebe Emmanuel Ezekiel, Nyiriza Makongoro Nyiriza, Masso Gerald Jane na Misogalya Isaac Kilangi Kassile.


                                     WAKIENDELEA kushukuru.

Nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Mwanza ni Salum Mohamed Chima, Yusuph Mwandami Gwayaka, Bertha Peter Nakomolwa na Philemon Josephat Kiemi.

Kwa upande wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kibaha Mjini ni Amina Ally Kobo, Lemmy Joel Ludovick na  Hamidi Rajabu Shebuge.

Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ilimteua Abdallah Ally Mtolea, kuwa Mgombea wa kiti cha Ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, imeiagiza Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), kurudia mchakato wa kupendekeza majina ya mgombea wa nafasi ya Mjumbe wa NEC.

Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kauli moja imetupilia mbali pingamizi zilizowekwa dhidi ya viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali na kuagiza viongozi hao waendelee na nyadhifa zao.

Pingamizi hizo ziliwekwa dhidi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Anthony Mwandu Diallo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Lindi Aisha Ally, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Salim Mohamed na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ngara George Jackson Rubagora.

Pamoja na kutupilia mbali pingamizi hizo, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC),  imewaagiza walezi wa mikoa yote ambayo viongozi wake waliwekewa pingamizi wakutane na wanachama na kukiunganisha chama.

Halmashauri Kuu ya CCM PIA, imemuagiza Zubeir Majaliwa, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Uvinza ambaye Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo  ilimsimamisha uanachama kuwasilisha rufaa yake kuanzia ngazi husika wakati adhabu yake ikiendelea.


                WAKITOA shukrani kwa Wajumbe wa NEC.

Aidha, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, imetoa adhabu ya kalipio kwa mwanachama wa CCM Hasnain Murji,  kutokana na kukabiliwa na makosa ya kimaadili.

Kikao hicho kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wake wa CCM Taifa, Rais Dk. John  Magufuli, kilipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na taarifa ya chama juu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa CCM ya mwaka 2015.

Pia, kikao hicho kimepokea taarifa kuhusu masuala ya maadili, kimepokea na kuridhia marekebisho ya kanuni mpya za fedha na mali za chama na jumuiya zake na kimepokea na kuridhia uteuzi wa wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa CCM.

No comments