Breaking News

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAWATAKA WAAJIRI NCHINI KUWAPATIA HUDUMA STAHIKI WATUMISHI WA UMMA WENYE ULEMAVU ILI WAWEZE KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KIKAMILIFU.


1.   NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Dorothy  Mwaluko, akifungua kikao kazi  cha Watumishi wa Ofisi ya Rais, Utumishi cha kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo Jijini Dodoma leo Desemba 3, 2018.    


                                  Na Mwandishi Wetu, Dodoma

OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetoa wito kwa waajiri nchini, kuwapatia huduma stahiki watumishi wa umma wenye ulemavu kwa mujibu wa Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu wa mwaka 2008 kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Wito huo umetolewa leo Desemba 3, na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dorothy Mwaluko, wakati wa kikao kazi  cha Watumishi wa Ofisi ya Rais, Utumishi cha kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo Jijini Dodoma.
1.   DOROTHY,  akimkabidhi Mkurugenzi wa Sera, Ofisi ya Rais, Utumishi,  Agnes Meena, Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu wa mwaka 2008  ili aweze kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa mwongozo huo katika taasisi za umma nchini. 

Mwaluko alisema, walemavu kama walivyo binadamu wengine, wana wajibu wa kutoa mchango katika maendeleo ya taifa, hivyo ni wajibu wa waajiri wote nchini kuwapatia huduma zinazostahili ili waweze kutimiza wajibu wao.

Alifafanua kuwa, watumishi wa umma wenye ulemavu hawana tofauti na watumishi wengine isipokuwa wana mahitaji yao ya msingi ambayo usipowapatia yanakwamisha utendaji kazi wao, hivyo waajiri hawana budi kuzingatia mahitaji ya kundi hilo ambalo baadhi ya waajiri hulisahau.


1.   OFISA Tawala Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi, Mwanaamani Mtoo, akiwasilisha mada kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu katika utumishi wa umma wakati wa kikao hicho.


Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Watumishi wenye Ulemavu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Elibariki  Kahungya, alisema, ofisi kama msimamizi wa Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu wa mwaka 2008, inawawezesha watumishi sita waliopo wenye ulemavu kupata huduma muhimu kama mwongozo unavyoelekeza ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kahungya amezitaja huduma zinazotolewa kuwa ni pamoja na chombo cha usafiri (bajaji), mafuta ya vyombo vya usafiri kila wiki, vifaa vya kuwezesha kusikia, mafuta ya ngozi na posho ya lishe na dawa kwa mtumishi mwenye ulemavu usioonekana.


1.   NAIBU Katibu Mkuu,  Dorothy, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Rais, Utumishi baada ya kufunga kikao kazi cha kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo Jijini Dodoma.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeungana na wadau wengine duniani kuadhimisha Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 03 ya kila mwaka. Kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Niwawezeshe  Wenye Ulemavu na Kuwajumuisha kwa Usawa.

No comments