Breaking News

RAIS DK. JOHN MAGUFULI AHITIMISHA MJADALA WA WANANCHI WALIOJENGA KWENYE HIFADHI YA BARA BARA KUTAKA KULIPWA FIDIA.  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli, akihotubia wananchi katika hafla ya uwekaji Jiwe la Msingi la Ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro Kuanzia Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa kilometa 19.2 .Hafla iliyofanyika Kimara Jijini Dar es Salaam. Leo Desemba 19,2018. (Picha zote na Ikulu).
                        Na Thomas Mtinge

RAIS Dk. John Magufuli, amewataka wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi waliovunjiwa nyumba zao wakati wa upanuzi wa bara bara kwamba watalipwa fidia.

Alisema, Serikali haitalipa fidia kwa mtu yeyote aliyejenga katika eneo la hifadhi ya barabara kwa mujibu wa sheria.

“Kuna wanasiasa wanataka waonekane wao ndio wanawatetea wananchi na wanasema Serikali itoe fidia, nataka niwaambie ndugu ukivamia barabara unatafuta umasikini, fidia haipo, fidia haipo, narudia fidia haipo,” alisisitiza.

Magufuli na kuwataka Watanzania kote nchini kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kujenga makazi.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli, aliyoitoa leo Desemba 19, 2018, wakati akihutubia wananchi katika hafla ya kuweka jiwe la msingi  jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro Jijini Dar es Salaam katika sehemu ya kuanzia Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa Kilometa 19.2, imehitimisha mijadala huo usiokuwa rasmi.

Upanuzi huo utahusisha kuongeza njia za magari kutoka mbili zilizopo sasa hadi nane, kujenga madaraja sita na makalavati 36, na kujenga barabara ya juu (Flyover) katika eneo la Kibamba CCM kwenye makutano ya barabara inayotokea Bunju na barabara ya kwenda hospitali ya Mloganzila.

RAIS Dk. John Magufuli, akikata utepe  na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa pamoja na viongozi wa dini wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro Kuanzia Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa kilometa 19.2.

Aidha, Rais Magufuli alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kulipa kodi na kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha kodi inayokusanywa inasimamiwa vizuri kwa kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, kuendeleza elimu, afya na kuboresha upatikanaji wa maji ukiwemo mkoa wa Dar es Salaam ambao kwa sasa unapata maji kwa asilimia 75.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwaonya Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam waliokuwa wakichelewesha kuanza kwa ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi kutokana na kubishana juu ya mkandarasi wa kukijenga.

“Nilikuwa nawafuatilia jinsi mnavyobishana na leo mngekuwa bado mnabishana nilipanga nitangaze kuondoa fedha za ujenzi wa kituo hicho sh. Bilioni 50 na kupeleka mahali pengine…ndugu zangu viongozi naomba tutangulize maslahi ya wananchi, sio maslahi yetu binafsi,” alisisitiza Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli, aliwapongeza wananchi wa Dar es Salaam kwa kupatiwa mradi huo mkubwa na kubainisha kuwa pamoja na barabara, hiyo Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuboresha miundombinu ya Dar es Salaam ambapo barabara zenye jumla ya kilometa 212 zinajengwa kwa gharama ya sh. Bilioni 660.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale, alisema barabara ya Morogoro ni lango kuu la usafiri kati ya Jiji la Dar es Salaam lenye bandari kuu na mikoa mingi ya Tanzania Bara na nchi jirani.

Alisema  kwamba upanuzi wake utasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa magari takribani 50,000 yanayopita katika barabara hiyo kwa siku na utaokoa muda kutoka saa tatu zinazotumika kupita eneo hilo kwa sasa hadi nusu saa.

DK.. Magufuli,  akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi  Mfugale, akitoa maelezo ya mradi wakati wa hafla  ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro Kuanzia Kimara hadi Kibaha. 

Alisema kuwa upanuzi wa barabara hiyo utafanyika kwa muda wa miezi 30 kuanzia  Julai 21, 2018 na utagharimu sh. Bilioni 141.56, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania.

Mapema Spika wa Bunge, Job Ndugai alimpongeza Rais Magufuli, kwa namna Serikali inavyosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na kumhakikishia kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi hizo zenye maslahi makubwa kwa Taifa.

Pia, Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wamemshukuru Rais Magufuli, kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika mkoa huo ikiwemo kutatua tatizo la maji, kuimarisha miundombinu ya barabara na reli, kununua ndege na kuboresha uwanja wa ndege na kuboresha huduma za afya na elimu.

Naye Wakati huo huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema Serikali itaanza kutekeleza sheria ya kudhibiti uzito wa magari barabarani kuanzia Januari 2019 ili kuokoa uharibifu mkubwa wa barabara unaojitokeza katika barabara nyingi hivi sasa.

No comments