Breaking News

RAIS DK. MAGUFULI ATOA KAULI NZITO KWA JESHI LA POLISI.


AMRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Rais Dk. John Magufuli, akihotubia viongozi wa majeshi, serikali pamoja na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika hafla ya kufunga mafunzo ambapo jumla askari 513 wakiwemo maofisa wa 120 wa Polisi na wakaguzi wasaidizi 393 walihitimu katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini Jijini Dar es salaam jana Desemba 21, 2018. Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na igp simon Sirro. (Picha zote na Ikulu).


                                    Na Mwandishi Wetu

RAIS Dk. John Magufuli, amesema hatarajii kuona Jeshi la Polisi nchini, likiendeleza mambo yanayotia doa utendaji kazi wa Polisi yakiwemo kupokea rushwa, kunyanyasa watu, kubambikiza kesi na utovu wa nidhamu, badala yake amewataka kuzingatia kiapo chao na ujumbe uliomo kwenye wimbo wa jeshi hilo.

Alitoa kauli hiyo jana Desemba 21, 2018, wakati akifunga mafunzo kwa Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania katika shrehe zilizofanyika kwenye Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa muda wa miezi 6 ambapo jumla ya askari 513 wakiwemo Maafisa wa Polisi 120 na Wakaguzi Wasaidizi 393 walihitimu.BAADHI ya wahitimu hao ambao ni maofisa wakaguzi wapya, wakimsikiliza Magufuli (hayupo pichani).

“Mkisikia sisi viongozi tunasema nchi ina amani na utulivu, basi mjue tunajivunia uwepo wa Jeshi la polisi, kwa hivyo nawapongeza sana kwa jinsi mnavyopambana na uhalifu, mlipambana kule Kibiti mpaka askari wenzenu walipoteza maisha, natambua mchango wenu na nawapenda sana,” alisema Magufuli.

Maguful,i aliwapongeza Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi kwa kuhitimu mafunzo hayo na amewataka kwenda kuwahudumia wananchi vizuri na kuwasimamia askari watakaowaongoza kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.


MAOFISA na Wakaguzi wapya wa Jeshi la Polisi wakitoa salamu ya heshima walipopita mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Rais Dk. John Magufuli (hayupo pichani) katika hafla hiyo.

Katika hafla hiyo, Magufuli, alikubali ombi la sh. Milioni 700 lililotolewa na Mkuu wa chuo hicho (DCP) Anthony Rutashuburugukwa kwa ajili ya kukarabati majengo ya chuo na kuagiza fedha hizo pamoja na fedha nyingine kiasi cha sh. Bilioni 7 ambazo ni kati ya sh. Bilioni 10 alizoahidi kutoa kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya askari Polisi zitolewe kwa jeshi hilo ndani ya kipindi cha wiki moja.

Aidha, Rais Magufuli, aliwatia moyo askari Polisi wanaotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu na amewataka Maafisa wa Polisi waache kuwakatisha tamaa askari wanapotekeleza majukumu yao ikiwemo kuwaamrisha  wa vyeo vya chini wawaachie watuhumiwa wanaowakamata, kuwaweka askari mahabusu na kuwakataza kutekeleza majukumu yao kwa kigezo cha kutokuwa na kibali.
RAIS Dk. Magufuli, akikagagua na kuangalia baadhi ya silaha zilizokamatwa na Jeshi la Polisi ambazo zilitumika katika matukio mbalimbali ya kiualifu hapa nchini. Kulia ni IGP Sirro 

“Nafahamu kuna askari walichomwa visu wakati wanawakamata watuhumiwa, naagiza askari hao watibiwe vizuri hata kama itahitajika kupelekwa nje na wale watuhumiwa waliowajeruhi wakamatwe na wapelekwe mahakamani,” alisisitiza Magufuli.

Pia, Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa kitengo cha fedha cha Jeshi la Polisi Tanzania na amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kurekebisha dosari zilizopo pamoja na kuyalinda maeneo ya Jeshi la Polisi yasimegwe, kuuzwa ama kuingia mikataba isiyokuwa na maslahi kwa jeshi hilo.


   BAADHI ya viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo.

Mapema akitoa taarifa kwa, Magufuli, IGP Sirro alimshukuru Rais  kwa kupatiwa fedha sh. Bilioni 10 kwa ajili ya kujenga nyumba 400 za makazi ya askari, kununuliwa magari 777 ambapo 497 wameshapatiwa, kupatiwa shilingi Bilioni 50.3 za kuwalipa wazabuni, kuboresha maslahi ya askari, kuwapandisha vyeo askari 3,089, kuajiri askari wapya 818 na ameomba nafasi zilizoachwa wazi na Maafisa na Askari waliostaafu zijazwe.


Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alimshukuru Magufuli kwa usimamizi wake wa karibu kwa Jeshi la Polisi na ameahidi kuwa polisi wataendelea kutekeleza majukumu yao ya usalama wa raia na mali zao kikamilifu na kwa weledi.

No comments