Breaking News

SHILINGI BIL. 222 ZIMELIPWA KWA WAKULIMA WA KOROSHO-MAJALIWA.


WAZIRI  Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara akiwa njiani kwenda Ruangwa, leo Desemba 30, 2018. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).


Na Mwandishi Wetu, Mtwara

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema jumla ya sh. Bilioni 222 zimelipwa na Serikali kwa wakulima wa zao la korosho na kuwataka wakulima wawe na subira.

Alisema wakulima walioanza kulipwa ni wale wenye kilo zisizozidi kilo 1,500 huku wenye zaidi ya kilo 1,500 na kuendelea Serikali inaendelea na uhakiki kisha watalipwa.

”Fedha zipo, hakuna mkulima ambaye atapoteza haki yake wote watalipwa. Tunaendelea na uhakiki kwa wale wenye korosho nyingi ili kubaini kama hawajanunua kangomba,” alisema.
MAJALIWA, akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Jilly Maleko,  wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Mtwara. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge.Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Desemba 30, 2018, alipozungumza na wananchi wa Kijiji cha Nandagala ‘A’ baada ya kufungua ofisi ya CCM kata ya Nandagala.

Alisema baadhi ya watu wamekutwa na kilo zaidi ya 1,500 na wameshindwa kuonyesha mashamba yao ya mikorosho, hali inayodhihirisha kwamba wamenunua kupitia kangomba.

Majaliwa, alisema baadhi ya waliokutwa na korosho nyingi ni vijana wadogo ambao hawana hata uwezo kifedha hivyo Serikali itahakikisha inawakamata watu wanaowatuma.
KASSIM Majaliwa, akislimiana na viongozi wa mkoa wa Mtwara wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa mkoa huo.

Alisema lengo la Serikali inayoongizwa na Rais Dk. John Magufuli, ni kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo chao, hivyo biashara ya kangomba lazima ldhibitiwe.

Waziri Mkuu ambaye leo alianza ziara yake ya kikazi wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi alisema kazi ya ulipaji kwa wakulima wa korosho lnaendelea, wakulima wawe na subira.

Serikali iliamua kununua korosho zote za mwaka huu baada ya kubaini wafanyabiashara wamepanga kuwadhulumu wakulima kwa kupanga kununua kwa bei ndogo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alitembelea eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Matambalale wilayani Ruangwa ambapo aliwataka wahakikishe ujenzi unakamilika.


WAZIRI Mkuu, akisalimiana na wananchi wakati alipowasili katika Kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa.

Aliwataka wananchi wa kata hiyo kushirikiana na kuhakikisha wanachangia nguvu kazi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili mwakani wanafunzi waanze kusoma.

”Tunataka tuondoe dhiki ya watoto wetu kutembea umbali mrefu hadi Namichiga kutafuta elimu, tunataka watoto wetu wote wasome katika maeneo yaliyo karibu na makazi yao,” alisisitiza Majaliwa.

Waziri Mkuu huyo alisema, wanafunzi zaidi ya 200 wamefaulu na hawana pa kwenda hivyo ni lazima ujenzi wa shule zote za sekondari za Matambalale, Chibura na Ruchelegwa ukamilike.

Kwa mujibu wa Majaliwa, hadi Januari 10, 2019 shule hizo zote lazima ujenzi wake ukamilike ili wanafunzi waanze kusoma, hivyo viongozi washirikiane na wananchi kukamilisha ujenzi.

No comments