Breaking News

WATUMISHI WA UMMA ZINGATIENI MAADILI NA NIDHAMU YA KAZI-MARY.

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akizungumza na watumishi wa Idara ya Ukuzaji Maadili ya wizara yake jana Desemba 21, 2018 Jijini Dodoma  kwa lengo la kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara na kuhimiza uwajibikaji.

                                    Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WWATUMISHI wa Umma nchini wametakiwa kuzingatia maadili na nidhamu ya kazi kwani ndio msingi na nyenzo kuu itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Hayo yalisemwa jana Desemba 21, 2018 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, alipokutana na watumishi wa Idara ya Ukuzaji Maadili ya wizara yake kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji.

Dk. Mary alisema, maadili mema kwa watumishi wa umma ndio kitovu cha utumishi wa umma hivyo ameitaka Idara ya ukuzaji maadili kuhakikisha watumishi wa umma wanazingatia misingi ya maadili mema na nidhamu katika utendaji ili waweze kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.

Alifafanua kuwa mtumishi wa umma akiwa na maadili mema, utendaji kazi wake utaimarika pia utii, heshima na adabu vitaongezeka hivyo atakuwa mchapakazi hodari na anayezingatia weledi.

“Mtumishi wa umma anatakiwa ajitambue katika mwenendo wake, azingatie mavazi ya heshima mahala pa kazi, awe na lugha nzuri yenye staha kwa wateja ili awe kioo na mfano mzuri wa kuigwa katika jamii.

“Idara ya Ukuzaji Maadili kutengeneza mkakati madhubuti  wenye ubunifu utakaowezesha kutoa elimu ya maadili kwa umma ili jamii itambue umuhimu wa maadili mema mahala pa kazi, na ameongeza kuwa Idara hiyo iweke utaratibu wa kuzitambua taasisi na watumishi wa umma wanaozingatia maadili ya kazi kwa kuwapa tuzo lengo likiwa ni  kuwapa motisha ya utendaji kazi,” alisisitiza Dk. Mary.
MKURUGENZI wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Fabian Pokela (kulia), akifafanua majukumu ya Idara yake kwa Naibu Waziri Dk. Mary (hayupo pichani).

Aliainisha kuwa, watumishi wa umma wakiwa waadilifu  na wazalendo, watawezesha kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma.

Aidha, Naibu Waziri huyo, aliitaka Idara hiyo kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli, kwa vitendo katika kuhimiza uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini ili utumishi wao uwe na tija katika maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Fabian Pokela, alisema kuwa, majukumu ya Idara hiyo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni ukuzaji maadili katika utumishi wa umma na ufuatiliaji wa Uzingatiaji wa Maadili katika utumishi wa umma sanjari na ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi yanayohusu ukiukwaji wa maadili katika Utumishi wa Umma.

Pokela alifafanua kuwa, jukumu la sehemu ya ukuzaji maadili ni kuhakikisha kuwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla wanapata uelewa kuhusu maadili ya utumishi wa umma kupitia kampeni za uhamasishaji, maonesho mbalimbali, vipeperushi, majarida mbalimbali, semina, warsha, mikutano na mafunzo ya muda mfupi.

BAADHI ya watumishi wa Idara ya Ukuzaji Maadili,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa (hayupo pichani)..

Mkurugenzi huyo alisema Idara yake pia imeandaa vipindi vya redio na televisheni vitakavyotoa elimu kwa umma juu ya maadili mema mahala pa kazi na kuhimiza uadilifu kwa Watendaji Wakuu wa  Taasisi na  mtumishi wa umma mmoja mmoja.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, aliitembelea Idara ya Ukuzaji Maadili ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika Idara na Vitengo vya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhimiza uwajibikaji.

No comments