Breaking News

WAZIRI KALEMANI AIBUA SHANGWE IPARAMASA.WAZIRI wa Nishati Dk. Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Iparamasa, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, akiwa katika ziara ya kikazi juzi Desemba 21, 2018 ambapo pia aliwasha rasmi umeme kijijini hapo. (Picha zote na Veronica Simba).

Na Veronica Simba – Chato

WAZIRI wa Nishati Dk. Medard Kalemani, amewasha umeme katika Kijiji cha Iparamasa, Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Kwa umeme huo, kulileta matumaini mapya kwa wananchi wa kijiji hicho kutokana na kukosa huduma hiyo muhimu kwa pikindi kirefu hali iliyoibua shangwe na nderemo kwa kujawa na furaha.

Umeme huo katika kijiji hicho, uliwashwa  juzi Desemba 21, 2018 wakati Waziri Kalemani, akiwa katika ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuzungumza na wananchi.
WANANCHI wa Kijiji cha Iparamasa wilayani Chato, wakiwa wamejipanga kumpokea na kusalimiana na  Waziri Dk. Kalemani, (mwenye shati la bluu), alipowasili kuzungumza nao na kuwasha rasmi umeme kijijini hapo, akiwa katika ziara ya kikazi.

Akizungumza na wananchi, Waziri Kalemani, aliwataka wautumie umeme huo katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuendeshea viwanda vidogovidogo vya kusaga na kukoboa nafaka na kadharika.

“Umeme huu siyo kwa ajili ya kuwasha taa tu. Ni umeme unaotosha kwa matumizi ya viwanda, hivyo basi utumieni ipasavyo ili kuboresha maisha yenu,” alisisitiza Waziri.DK. Kalemani (mwenye shati la bluu), akijumuika kucheza na wananchi wa Kijiji cha Iparamasa wilayani Chato, wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo.

Aidha, aliwahamasisha wananchi ambao hawajalipia gharama za kuunganishiwa umeme, wafanye waendelee kulipa ili waunganishiwe kwakuwa huduma hiyo ni muhimu.Pia, aliwashauri wananchi wenye matumizi madogo madogo ya umeme, kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ili kuondokana na gharama za kufunga nyaya katika nyumba zao.

Sambamba na hilo, alitoa vifaa vya UMETA 50 bure kwa ajili ya wazee na wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kufunga nyaya za umeme.

“Mbali ya vifaa 250 vya UMETA ambavyo hutolewa bure kila eneo tunapowasha umeme kwa ajili ya wananchi watakaojitokeza mwanzoni kulipia na kuunganishiwa umeme, mimi nikiwa kama Mbunge wenu, nawaongezea vifaa vingine 50 bure ili vifungwe kwa wazee na wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za kuunganishiwa umeme,” alisema.
MZEE Yohana Masanyiwa, akisoma risala kwa kwa Waziri Kalemani, (hayupo pichani).

Kwa upande wa wachimbaji wadogo wa madini wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo, Waziri Kalemani, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato, alisema alishaagiza mashine umba (transfoma) kubwa saba ambazo zitafungwa ili kuwawezesha kuendesha mitambo yao bila shida.

Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Geita, Mhandisi Joachim Ruweta, mpaka sasa jumla ya wateja 331 wameunganishiwa huduma ya umeme kwa Wilaya ya Chato, ambapo 16 kati yao ni kutoka Kijiji hicho cha Iparamasa.

“Waliolipia huduma ya kuunganishiwa umeme katika Kijiji cha Iparamasa ni 36, lakini waliopata huduma ni 16. Kazi ya kuunganishia wateja wengine inaendelea,” alifafanua Mhandisi Ruweta.
MKUU wa Wilaya ya Chato, Mhandisi Msafiri Mtemi, akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme kijiji cha Iparamasa, Wilaya ya Chato.

Waziri Kalemani, yuko katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Kanda ya Ziwa hadi Januari 2, mwakani.

No comments