Breaking News

BARAZA LA MAWAZIRI LARIDHIA KUTOZA VATI KWA KIWANGO CHA ASILIMIA SIFURI KWA UMEME UNAOUZWA NA TANESCO KWENDA ZECO NA KUFUTA DENI.


 RAIS Dk. John Magufuli, akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika jana Januari 21, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Ikulu).

                                   Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Mawaziri limeridhia utozwaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye umeme unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).

Pia, limeridhia kufuta malimbikizo ya deni la kodi ya VAT lililofikia sh. Bilioni 22.9 kwa TANESCO kwenye umeme uliouzwa ZECO.

Baraza la Mawaziri limefanya uamuzi huo jana Januari 21, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam, katika kikao kilichoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi na Mawaziri.

Akizungumza baada ya kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli alisema baada ya kufanya uamuzi huo, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango, atawasilisha marekebisho madogo ya sheria ya VAT, sura ya 148 kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ili umeme unaouzwa Tanzania Zanzibar utozwe VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri.

“Kwa hiyo madeni yatakayokuwa yanadaiwa kwa Zanzibar ni yale madeni ya kulipia umeme, umeme wametumia kiasi fulani wanalipa kama wanavyolipa wa maeneo mengine…kwa mfano wanavyolipa Dar es Salaam, suala la kutoza VAT sasa halipo, na katika hilo kwa sababu kulikuwa na deni ambalo lilikuwa limefika sh. Bilioni 22.9, sisi Baraza la Mawaziri tutapeleka mapendekezo Bungeni.

“Mapendekezo hayo ni  kwamba deni hilo lisamehewe kwa sababu lipo ndani ya bajeti ya mwaka huu wa 2018/19, kwa hivyo litapunguza mapato yatakayotakiwa kukusanywa na Serikali,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar Dk. Shein alisema pamoja na kuridhia utozaji wa VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri, Baraza la Mawaziri pia limekubaliana kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ataitisha vikao vya kuzungumzia masuala ya Muungano kila mara kunapokuwa na hoja ya masuala ya Muungano ili kujadili na kutoa uamuzi.

“Tungependa sana mambo haya yafanyike vizuri kwa sababu pande mbili za Muungano zinatuhusu sote, hili ni muhimu kwa sababu mambo yakikusanyika mengi wananchi wanahisi hatusaidii jitihada zao.

“Kwa hivyo tumeridhia kuwa masuala ya Muungano ambayo yapo chini ya Makamu wa Rais, wakae pamoja wayajadili ili yapate uamuzi wa pande zote mbili,” alisema  Dk. Shein.

Wakati huo huo, Rais Dk. John  Magufuli alimuapisha  Anjellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji.
Waziri Angellah, aliapishwa kabla ya kuanza kwa kikao cha Baraza la Mawaziri, kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza hilo yaliyofanywa na Rais Magufuli, Januari 8, 2019 ambapo  Angellah, aliyekuwa Waziri wa Madini aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji.


DK. John Magufuli, akimuapisha Angellah Kairuki, kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Ikulu Jijini Dar es Salaam.
 RAIS Magufuli (kushoto) akifurahia jambo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, mara baada ya kutoka kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (KULIA), akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) mara baada ya kutoka kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika jana Ikulu, Dar es Salaam. Kushoto ni Rais  Magufuli.
 DK. Magufuli akizungumza na wanahabari(hawapo pichani).
 MAGUFULI, akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri. Kulia ni  Dk. Ali Mohamed Shein.RAIS Dk. John Magufuli, akiagana na Rais wa Zanzibar Dk. Shein mara baada ya kuzungumza na wanahabari Ikulu Jijini Dar es Salaam.

No comments