Breaking News

BODI YA MISHAHARA YATAKIWA KUTOFANYA KAZI KWA MAZOEA KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE-DK. MARY.


 NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, DK. Mary Mwanjelwa, akizungumza na watumishi na wajumbe wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi alipowatembelea  Ofisini kwao Makao Makuu ya bodi Jijini Dar es Salaam  leo Januari 15, 2015 kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. (Picha zote na James Mwanamyoto).
                              Na Mary Mwakapenda

WATUMISHI na wajumbe wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma wametakiwa kutofanya kazi kimazoea katika kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kuishauri Serikali namna bora ya kuoanisha na kuwianisha mishahara na masilahi ya watumishi wa umma nchini.

Hatua hiyo ina lengo la kuwavutia na kuwabakiza watumishi katika Utumishi wa Umma ili waweze kuwahudumia vizuri wananchi katika Taasisi za Umma.


 KAIMU Katibu Mtendaji wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma, Mariam  Mwanilwa, akieleza  majukumu ya Bodi kwa Naibu Waziri Dk. Mary (kushoto).Hayo yamesemwa leo Januari 15, 2019 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akati akizungumza na watumishi na Wajumbe wa Bodi ya Mishara na Masilahi katika Utumishi wa Umma  Makao Makuu ya bodi hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu majukumu ya bodi na kujiridhisha namna bodi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.

Dk. Mary, alisema kuwa, yeye ni muumini wa ufuatiliaji hivyo atakuwa akifanya ziara za kushtukiza katika ofisi za Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kujiridhisha na utendaji kazi wa bodi hiyo, hivyo amewataka watumishi hao kubadilika na kuachana na utendaji kazi wa kimazoea ili bodi hiyo iwe na tija na manufaa kwa watumishi wa umma nchini.

Alisisitiza kuwa, pamoja na kuwataka watumishi na wajumbe wa bodi hiyo kufanya kazi kwa uzalendo, uaminifu na uadilifu lakini pia amewataka kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao ili kuisadia Serikali ya Awamu ya Tano kutimiza azma yake ya utoaji motisha kwa watumishi wa umma ili waweze kuwa na ari ya utendaji kazi.

 MWENYEKITI wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma, Donald Ndagula, akifafanua majukumu ya bodi yake katika kikao hicho. Kulia ni Dk. Mary.Aidha, Naibu Waziri huyo, aliwataka wajumbe wa bodi ambao ni wastaafu na wazoefu katika utumishi wa umma, kila mmoja kwa nafasi yake kutoa mchango utakaowezesha bodi kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kwa wakati, na kuongeza kuwa, yeye binafsi anaamini kwa uzoefu wa wajumbe wanaounda bodi hiyo, Serikali itapata ushauri bora wa kuoanisha na kuwianisha mishahara na masilahi ya watumishi wa umma nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma,  Mariam Mwanilwa, alisema kuwa, lengo la kuanzishwa kwa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma ni kuwa na chombo kimoja cha kuoanisha na kuwianisha mishahara na masilahi ya watumishi wa umma ili kuwa na mfumo endelevu unaoondoa malalamiko kuhusu masilahi miongoni mwa watumishi wa umma kwa lengo la kuwavutia na kuwabakiza watumishi katika Utumishi wa Umma.

 BAADHI ya watumishi wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri Dk. Mary (hayupo pichani).
Alieleza kuwa, hivi sasa bodi inafanya utafiti wa hali ya masilahi na uhusiano wake na mifumo ya upimaji wa utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na kuongeza kuwa, utafiti huo unafanywa ili kubaini uhusiano uliopo kati ya utoaji wa motisha mbalimbali na utendaji wa kazi kwa lengo la kuwavutia na kuwabakisha watumishi wa Umma.

Alifafanua kuwa, kwasasa hatua inayoendelea katika utafiti huo ni uchambuzi wa taarifa za utafiti huo, hivyo bodi inatarajia kuwasilisha taarifa hiyo serikalini ifikapo mwezi Februari, 2019.

 NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Dk. Mary Mwanjelwa, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe na watumishi wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma mara baada ya kumalizika kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi na Wajumbe wa Bodi hiyo ya Mishahara na Masilahi  katika  Utumishi wa Umma cha kuhimiza uwajibikaji  kilichofanyika Makao Makuu ya bodi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma, Donald Ndagula, alisema bodi yake inamtambua Dk. Mary, kama mlezi, hivyo amemhakikishia kuwa, imepokea nasaha, ushauri na melekezo aliyoyatoa na ameahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote.

Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 36 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na kuundwa kwa Hati ya Rais iliyotolewa kwenye Tangazo la Serikali Na. 162 la tarehe 3 Juni, 2011.

No comments