IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA YATAKIWA KUFUATILIA UTUNZAJI WA NAYARAKA ILI KUDHIBITI UVUJAJI WA SIRI ZA SERIKALI.
KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa Firimin Msiangi (kulia), akitoa ufafanuzi kwa Dk. Mary, kuhusu mifumo ya TEHAMA inavyofanya kazi katika utunzaji wa kumbukumbu na
nyaraka.ji katika idara hiyo.
Na Mary Mwakapenda, Dodoma
IDARA ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imetakiwa kufanya ufuatiliaji wa utunzaji
wa nyaraka na kumbukumbu katika taasisi zote za umma kwa lengo la kuondoa
tatizo la uvujaji wa siri za serikali.
Hayo yalisemwa leo Januari 25, 2019 na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dk. Mary Mwanjelwa, wakati akizungumza
na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa alipofanya ziara ya
kikazi katika ofisi hiyo Jijini Dodoma.
Ziara hiyo ina lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya
idara hiyo na kujiridhisha namna idara hiyo inavyotekeleza majukumu yake ya
kila siku.
Dk. Mary alisema, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ndiyo inayohusika
na masuala yote ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, hivyo inatakiwa ijiwekee
utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa namna ya nyaraka zinavyotunzwa na kushauri
namna bora ya utunzaji wa nyaraka hizo.
“Tujenge tabia ya kufanya ufuatiliaji wa miongozo tunayoitoa ili kuona kama
inatekelezwa inavyotakiwa kwani tusipofanya hivyo taasisi zinafanya inavyotaka
na matokeo yake ni kuvuja kwa siri za serikali,” alisisitiza Dk. Mary.
Naibu Waziri huyo alimtaka Mkurugenzi wa idara hiyo kuwa mkali na kuchukua
hatua za kinidhamu kwa taasisi zote za umma zinazoshindwa kutekeleza ipasavyo
jukumu la utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka na hatimaye kusababisha siri za
serikali kuvuja.
Aidha, aliipongeza idara hiyo kwa kutumia njia za kisasa za TEHAMA katika
kutunza kumbukumbu na nyaraka na kuwataka kuongeza kasi ya kuzihifadhi nyaraka
hizo kidigitali ili kuimarisha usalama wake.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi, ameyataja majukumu
ya idara yake kuwa ni pamoja na kuweka mifumo ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka
katika taasisi za umma.
Pia, kutoa ushauri juu ya utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka na
kuratibu mipango ya kutunza na kuhifadhi kumbukumbu muhimu katika taasisi za
umma, kuweka na kusimamia viwango vya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika
taasisi za umma.
Aliyataja majukumu mengine kuwa ni kukusanya na kuhifadhi nyaraka zenye
umuhimu kitaifa ili kulinda urithi andishi wa nchi yetu, kuandaa na kusimamia
utekelezaji wa miongozo ya kutunza na kuteketeza kumbukumbu katika taasisi za
umma.
Mengine ni kufanya tathmini ya kumbukumbu tuli (majalada yaliyofungwa) ili
kutambua yale yenye umuhimu wa kudumu kwa ajili ya kuyahifadhi, kuhifadhi
nyaraka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha upatikanaji na kulinda
nakala halisi na kukusanya, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za vitu vya waasisi
wa Taifa.
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ilianza kutekeleza majukumu yake
kama idara inayojitegemea tangu Julai, 2015 baada ya Rais wa Awamu ya Nne Jakaya
Kikwete, kupitisha muundo wa Idara Februari 12 2015.
NAIBU Waziri Dk. Mary Mwanjelwa (wapili kushoto), akishiriki kutoa nakala ya nyaraka ili
kuihifadhi katika mfumo wa TEHAMA. Anayemsaidia kutoa nyaraka hizo ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi.
DK. Mary (wapili kulia), akishuhudia baadhi ya kumbukumbu na nyaraka zilizohifadhiwa
katika majalada kwa ajili ya rejea ya kiofisi.
MTUNZA Kumbukumbu Msaidizi Joyce Maro (kushoto) akitoa maelezo Dk. Mry, juu ya
kumbukumbu zilizohifadhiwa katika Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu, Idara ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Dk. Mary Mwanjelwa (kulia), akisisitiza
namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za serikali ili kuondokana na
tatizo la uvujaji wa siri za serikali alipofanya ziara ya kikazi kuhimiza
uwajibikaji katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Jijini Dodoma leo
Januari 25, 2019. (Picha zote na James Mwanamyoto-UTUMISHI).
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Dk. Mary Mwanjelwa, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Idara ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa alipofanya ziara ya kikazi kuhimiza uwajibikaji
katika idara hiyo Jijini Dodoma.
No comments