KASI YA UJENZI MJI WA SERIKALI INARIDHISHA - WAZIRI MKUU *ASEMA SIKU YA MWISHO KUMALIZA UJENZI WA MAJENGO HAYO NI JANUARI 31, 2019.
Na
Irene Bwire, Dodoma
ZIKIWA zimepita siku 20 tangu akague
ujenzi wa Mji wa Serikali, Ihhumwa Jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
amesema ameridhishwa na ujenzi unaoendelea katika eneo lhilo.
Hata hivyo, alisema Kampuni ya
ujenzi ya Mzinga Holdings inahitaji kusimamiwa kwa karibu zaidi ili ikamilishe
ujenzi wa majengo yake kabla ya Januari 31, 2019.
“Nitakuja kukagua kazi na kupokea
funguo za ofisi siku hiyo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
MAJALIWA, akikagua Ujenzi wa
Mji wa Serikali kwenye eneo la Ihumwa.
Majaliwa, alitoa kauli hiyo leo Januari
16, 2019 mara baada ya
kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja katika eneo hilo la Ihumwa
lililoko km. 17 kutoka Dodoma mjini.
Waziri Mkuu ambaye alianza kukagua
ujenzi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais, ametembelea majengo ya wizara zote na
kubaini bado kuna changamoto zinazojitokeza kutokana na utendaji wa mazoea
miongoni mwa watumishi wa Serikali.
Akiwa katika jengo la Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri Mkuu alipokea malalamiko kutoka kwa
meneja mradi, Selemina Rwehumbiza, kwamba aliandaa certificate tangu Januari
13, lakini hadi sasa hajapata malipo.
WAZIRI Mkuu akikagua ujenzi.
Alisema alipofuatilia, alijibiwa na
mshauri mwelekezi kwamba wamepokea certificate hiyo jana jioni
(Jumatano, Januari 16, 2019.
“Kama kazi hii muhimu ya Rais, na
anayesimamia ni Waziri Mkuu inacheleweshwa hivi je, akija mwananchi wa kawaida
huko ofisini kwenu atachukua muda gani kupatiwa huduma?,” Waziri Mkuu alimhoji
Mshauri Mwelekezi wa mradi huo kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Mhandisi
Hilary Msaki.
“Huu ni mfano halisi wa malalamiko
yanayotoka huko nje kwamba Serikali haijibu barua za wananchi. Sasa nyaraka
kutoka hapa Mtumba inachukua wiki nzima kwenda mjini, na mtu bado hajajibiwa.
Sielewi ni kwa nini barua iende hadi mjini, wakati wakandarasi wako huku. Kwa
nini ninyi msipokee hizo nyaraka na kuzikimbiza mjini kisha mrudishe majibu
hapa site?”, alihoji Waziri Mkuu.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto) akizungumza
na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, wakati alipokagua ujenzi wa
jengo la Ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali unaojengwa eneo la Ihumwa.
Wapili kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi ya Tekinolojia, William Ole
Nasha na kushoto ni Katibu wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kuratibu
Mpango wa Serikali wa Kuhamia Dodoma, Meshack Bandawe.
“Kuanzia sasa, kazi zote mpokee
ninyi, na ninyi ndiyo mzipeleke huko mjini na kurudi na majibu hapa site
kwa wateja wenu, kwani wakandarasi wote wako hapa,” alisisitiza.
Akiwa katika eneo la Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri Mkuu alielezwa na Waziri
Ummy Mwalimu kwamba wana changamoto ya kutopatiwa taarifa za maendeleo ya
mradi.
“Tangu mradi unaze hatujapewa
taarifa hata moja, wakurugenzi wapo wanakuja, lakini mshauri mwelekezi hatupi
ripoti yoyote juu ya huu mradi,” alisema.
Alipohoji ni kwa nini taarifa
hazitolewi, Waziri Mkuu alibaini kuwa hata watu wa TEMESA pia hawakuwepo kwenye
zoezi hilo la ukaguzi. “Niliagiza TBA wahamie hapa, nao wameweka ofisi yao hapa
hapa. Nimeulizia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wako wapi, nikaambiwa wako
mjini. Ni kwa nini hawako hapa?” alihoji.
MAJALIWA, akizungumza na Saidi Kiwape (kushoto) ambaye ni fundi wa
kusuka nondo wakati alipokagua ujenzi wa Jengo la Ofisi za Wizara ya Nishati
kwenye eneo la Ihumwa. Wapili kulia ni Waziri wa Nishati, Dk. Medard
Kalemani, watatu kulia ni Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na
Ajira, Anthony Mavunde na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith
Mahenge.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi
wa tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, Waziri Mkuu alisema pamoja
na spidi anayoihimiza, bado wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia
ubora unaotakiwa (quality).
Alisema kwa ujumla kazi nyingi
zimeboreshwa tangu alipokagua mradi huo Desemba 27, mwaka jana. Aliitaka TBA
kwa kushirikiana na Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia
Dodoma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa/Mkurugenzi wa Dodoma wawasimamie wakandarasi na
hasa wale wa Mzinga ili kazi yao ikailike kwa wakati.
“Nimesisitiza katika kila site,
zile kazi ndogondogo zisizohitaji ujuzi au ufundi mkubwa, zigawiwe kwa vijana
ili kuongeza kasi lakini tuzingatie ubora wa kazi,” alisisitiza.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua ujezi wa tangi la maji lenye uwezo wa
kuhifadhi lita milioni moja za maji kwa ajili ya kuhudumia Mji wa
Serikali unaojengwa katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma. Katikati ni
Katibu wa Kikosi Kazi cha kitaifa cha
Kuratibu Mpango wa Serikali wa Kuhamia Dodoma, Meshck Bandawe.
Desemba 27, 2019, Waziri Mkuu
alikagua ujenzi wa eneo la Mji wa Serikali na kubaini kuwa baadhi ya
wakandarasi hawaendi na kasi inayotarajiwa na Serikali.
Siku iliyofuata aliitisha kikao cha
Mawaziri wote, Makatibu Wakuu na wakandarasi wao ili waeleze kazi hiyo
itakamilishwa lini. Kikao hicho alikifanyia hukohuko Ihumwa.
No comments