Breaking News

KESHO NI SIKU YA MAPINDUZI MATUKUFU ZANZIBAR.
VIJANA Halaiki wakifanya matayarisho ya mwisho kwa ajili ya  kilele cha Maadhimisho ya sherehe za kutimiza Miaka 55 ya Mapinduzi hapo Uwanja wa Gombani Chake Chake Pemba, kesho.

                          Na Othman Khamis Ame, Zanzibar


SIKU adhimu na muhimu  ya kumbukumbu ya Historia ya Visiwa vya Zanzibar iliyoleta Ukombozi wa Waafrika wa Zanzibar,  kupitia Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 imewadia  kutimia Miaka 55 keso Januari 12, 2019.

Matayarisho takriban yote yaliyofanywa kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe hizo yamefikia ukingoni ambapo kilele chake kitafikia katika Uwanja wa Michezo wa Gombani Chake Chake Pemba, wakati washiriki wote wa maadhimisho hayo hayo wameshawasili Kisiwani Pemba.
                     KIKOSI cha  Bendera kikiwa katika mazoezi.
  
Gwaride Rasmi la Vikosi vya Ulinzi na Usalama vitakavyopamba maadhimisho ya sherehe hizo limekamilisha matayarisho yake yaliyoshuhudiwa na Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar,  vikiongozwa na Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Raha iliyoje kwa wananchi watakaoshiriki maadhimisho hayo kutokana na ukakamavu mkubwa uliyoonyeshwa na vikosi hivyo kwenye matayarisho hayo ya mwisho ambayo imeonyesha muelekeo wa kufana.

 MOJA ya Vikosi vya Ulinzi vitakavyoshiriki kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Mapinduzi, KMKM kikipita mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa. (hawapo pichani).

Mbali ya gwaride hilo, sherehe hizo kama kawaida yake pia zitajumuisha maandamano, vikundi vya utamaduni kutoka wilaya mbali mbali nchini pamoja na vikundi vya Ulinzi vya Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kile Maalum cha Polisi Tarbushi.
Wakifanya tathmini ya maandalizi hayo ya mwisho katika ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP) ya uwanja wa michezo wa Gombani, wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa wameelezea kuridhika na hatua ya maandalizi hayo iliyofikiwa na washiriki wa sherehe hizo.

 WAJUMBE wa Kamati ya sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa wakiwa katika kikao cha maandalizi ya sherehe hizo.

Kilele cha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar cha Januari 12, kitatanguliwa na mkesha wa maadhimisho hayo utakaojumuisha ngoma za utamaduni zitazoambatana na fash fash katika uwanja wa michezo waTibirinzi Chake Chake Pemba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alikumbusha na kuhimiza washiriki wa sherehe hizo wakazingatia utaratibu wa muda uliowekwa  ili ratiba iende kwa wakati uliopangwa.
 BALOZI Ali Seif Iddi akisisitiza jambo kwa Wajumbe wa Kamati za Sekriteriet ya Kamati ya Sherehe ya Mapinduzi Zanzibar,  kuwajibika kwa majukumu yaliyombele yao katika kipindi hiki cha sherehe hizo. (Picha zote  na OMPR - ZNZ).


Balozi Iddi, alisema kwa vite wajumbe hao hawatokutana tena kipindi hiki cha kukaribia maadhimisho ya sherehe hizo za Mapinduzi  aliwataka wajumbe wa Kamati zote kauhakikisha kwamba wanatekeleza ipasavyo majukumu yao waliyopangiwa  kwa lengo la kuweka sawa changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza kipindi hiki.

No comments