Breaking News

MAGUFULI: SITACHOKA KUBADILI SAFU YA UONGOZI ENDAPO...*AANIKA HADHARANI DILI LA KUTAKA KUTOROSHA DHAHABU.
RAIS Dk. John Magufuli, akimuapisha Doto Biteko kuwa Waziri wa Madini. Kabla ya wadhifa huo, Biteko alikuwa Naibu Waziri wa Madini. Hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo Januari 9, 2019. (Picha zote na Ikulu).
             
                                   Na Thomas Mtinge

RAIS DK. John Magufuli, amesema hata choka kubadilisha mara kwa mara safu yake ya uongozi pindi atakapoona mambo hayaendi sawa.

Alisema, katika kubadilisha safu huko, hata muonea haya kiongozi yeyote hata kama ni rafiki yake, lakini kashindwa  kuwajibika ipasavyo katika nafasi aliyopewa.

“Kwakweli msishangae katika hili…niko tayari kubadili safu yangu mara kwa mara pindi nitakapoona mambo hayaendi kama nilivyokusudia. Nataka mkachape kazi muwatumikie wananchi, vinginevyo hata wewe Biteko ukishindwa utaondoka tu,” alisema Magufuli. 

Pia, Rais Dk. Magufuli, aliweka wazi jinsi lilivyofanyika dili la kutaka kutorosha nchini,  zaidi ya kilo 300 za dhabu na kumuagiza IGP Simon Sirro, kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika na tuhuma hizo wakiwemo askari Polisi nane.

Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo leo Januari 9, 2019 baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua jana pamoja na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma aliwateua hivi karibuni ambapo hafla ya kuwaapisha ilifanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali yake.

“Sitaki kuingilia uchunguzi wenu, lakini kwa taarifa nilizonazo, watuhumiwa wale walishikwa Januari 4, Wilayani Misungwi, walirudishwa mjini Mwanza na kikosi cha polisi nane. Wakapelekwa Central wala hawakuingizwa ndani.

"Watuhumiwa walikuwa kwenye gari wakawa wanajadili namna ya kuwapa hela, wakaambiwa watawapa Bilioni 1," alisema Magufuli.

Kwa mujibu wa Magufuli, watuhumiwa hao walitoa rushwa ya sh. Milioni 700 na kubakisha Milioni 300 ambazo polisi waliahidiwa kuwa wangepewa wakifika Sengerema.

Alisema baada ya ahadi hiyo, Polisi hao waliendelea kuzunguuka na watuhumiwa hao kwa kutumia gari na mafuta ya serikali na wakavuka nao Kigongo Ferry kuelekea Sengerema.

Magufuli alisema taarifa za kinteilijensia zikawa zimemfikia hivyo, akatoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongera na Mkuu wa Wilaya wa Sengerema kuwafuatilia watu hao na wakamatwe mara moja.
“Polisi waliohusika walikuwa wakitembea na watuhumiwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi na kuwaacha watuhumiwa ndani ya gari la Polisi bila RPC kujua.

MAGUFULI, akimuapisha Dorothy Mwaluko, kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji). Kabla ya wadhifa huo, Dorothy, alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 


“Muda wote huo walikuwa wakijadiliana jinsi ya kupeana rushwa na walikuwa wakila pamoja kabla ya kuanza kuwasindikiza waweze kutorosha dhahabu huku wakiwa wameshapewa sehemu ya fedha za rushwa walizoomba,” alisema Magufuli.

Hata hivyo, alisema dili hilo liliota mbawa baada ya kikosi kingine cha polisi kuweka mtego mbele ya safari yao, hivyo kuwakamata na kuwanyang’anya bunduki na kuwafikisha katika kituo cha polisi kwa hatua zaidi.

Kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa hao mkoani Mwanza, Magufuli amempongeza IGP Sirro, kwa kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi lake la Polisi.

“IGP nakupongeza sana kwa kazi nzuri ulioifanya. Hakika nakupongeza umefanya kazi nzuri sana kwa kushirikiana na jeshi lako. 

“Nilikuwa nafuatilia kwa karibu, ungeyumba na wewe mpaka dakika hii ingekuwa basi tena, lakini niliikia hata Yule polisi aliyekuwa anaongoza utoroshaji ushamng’oa wadhifa wake na kumuweka ndani sasa anavaa viatu visivyokuwa na kamba,” alisema.


Dk. Magufuli akimuapisha Dk. Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya). Kabla ya wadhifa huo, Dorothy, alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Alisema amechukizwa na kitendo hicho cha  rushwa kilichofanywa na askari wachache wasiowaaminifu ambacho kimelenga kulidhalilisha na ku kulichafua Jeshi la Polisi.

“Majeshi yetu bado yako imara na yanafanya kazi nzuri sana. Hili doa la wachache haliwezi kuchafua majeshi yetu, ninawapongeza sana kwa kazi nzuri,” alisema Magufuli.
Katika hatua nyingine, Mgufuli alieleza kutoridhishwa na utendaji wa Wizara ya Madini kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo rasilimali zake.

Alisema haridhishwi na utendaji wa widhara hiyo hususani katika udhibiti wa utoroshaji wa madini na hivyo amemtaka Waziri aliyeteuliwa Doto Biteko na taasisi zilizo chini ya wizara yake kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu ya Tanzania kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini ili kudhibiti utoroshaji na kuiwezesha Benki Kuu kuwa na hifadhi ya dhahabu.

“Tumewaruhusu wawekezaji na wachimbajiwadogo wachimbe dhahabu, Je Wizara ya Madini mmeshajiuliza dhahabu inayochimbwa inauzwa wapi?.

“Na je kama wanachimba na wanauza sisi tunapata asilimia ngapi?.  Hili suala ni la Wizara ya Madini, halikuwa suala la Bunge kujiuliza, wala halikuwa suala la Waziri Mkuu au Rais kujiuliza.

“Kwenye sheria ya madini nina hakika kuna mahali imeelekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuuzia madini, je vimeanzishwa vituo vingapi? viko wapi? Kwa sababu vingeanzishwa vituo hivi tungejua dhahabu inayosafirishwa, wapi imeuzwa  na inawezekana tungekuwa na taarifa za kila wiki, lakini hakuna,”.  alisisitiza Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amewaonya viongozi wa Serikali ambao wamekuwa wakilumbana badala ya kufanya kazi na amesema vitendo hivyo vikiendelea hatasita kutengua uteuzi wao na kuteua viongozi wengine watakaofanya kazi bila malumbano.

Mapema wakitoa salamu, Spika wa Bunge Job Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamisi Juma wamewapongeza viongozi walioteuliwa na wamewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, na kwamba Bunge na Mahakama zitatoa ushirikiano kwao.

Nae Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza viongozi walioteuliwa na kubainisha kuwa Serikali inaamini kuwa wataongeza nguvu katika utekelezaji wa ahadi ambazo imewaahidi wananchi hadi kufikia 2020.


Walioapishwa na vyeo katika mabano ni Doto Mashaka Biteko (Waziri wa Madini), Zainab Abdi Seraphine Chaula (Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Afya), Dorothy Aidani Mwaluko (Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji).

Arch. Elius Asangalwise Mwakalinga (Katibu Mkuu Ujenzi), Faustine Rweshabura Kamuzora (Katibu Tawala Mkoa wa Kagera), Dorothy Onesphoro Gwajima (Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia afya na Dk. Francis Kasabubu Michael (Naibu Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora).

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma walioapishwa ni Mwenyekiti wa Tume Jaji Mstaafu Steven James Bwana), na Makamishna 6 ambao ni George Daniel Yambesi, Yahaya Fadhili Mbila, Hadija Ali Mohamed Mbaraka, Immaculate Peter Ngwale, Daniel Ole Njoolay na John Michael Haule.

No comments