Breaking News

RAIS MAGUFULI AZUNGUMZIA UMUHIMU WA DHANA YA KUJITEGEMEA * ASEMA DUNIANI HAKUNA CHA BURE.

 RAIS  Dk. John Magufuli,  akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhandisi Isaack Kamwelwe,  wakipewa maelezo na  Rubani Patrick kuhusu, wakati ndege ya pili ya Airbus A220-300 walipoipokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.


                                       Na Thomas Mtinge

RAIS Dk. John Magufuli, amesema kwamba hakuna nchi Duniani iliyoendelea kwa kutegemea misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali.

Alisema, nchi lazima ijitegemee kwani dhana ya kujitegemea kama ilivyo kwa Tanzania, ndio itakayo tuokoa.
“Hakuna nchi dunia iliyoendelea kwa kutegemea misaada…haipo. Dhana ya kujitegemea ndani ya Tanzani ndio itakayotuokoa.

“Cha bure hakipo. Misaada inalemaza…tunahitaji misaada itakayotuwezesha kujitegemea,” alisisitiza Rais Dk. Magufuli.
Rais Magufuli, alitoa kauli hiyo katika mapokezi ya ndege mpya aina ya Airbus A220-300 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Ndege hiyo ni ya pili ya aina ya Airbus 220-300 kununuliwa na Serikali kwa ajili ya ATCL na ni ndege ya 6 kuwasili hapa nchini kati ya ndege 7 ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imezinunua kwa lengo la kuimarisha usafiri wa anga, kukuza utalii, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.

 WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na mkewe Mama Mary Majaliwa wakiwa na viongozi wengine mbalimbali wakishuka kutoka katika ndege ya pili ya Airbus A220-300 ilipowasili na kupokelewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Hafla ya mapokezi ya ndege hiyo, ilifanyika jana Januari 11, 2019 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal One) Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na kudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa  Chama Tawala (CCM), Serikali yake na wananchi wa kada zote.

Aidha, katika hafla hiyo, Rais Magufuli, aliutaka uongozi wa ATCL kupunguza matumizi ya hovyo ili waweze kupata faida nzuri za uendeshaji wa shirika hilo.

“Zamani ndege ilikuwa ikisafiri kwenda nje kufuata nguo za kwenye maduka ya watu Fulani…hiyo sasa muache,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumzia kuhusu watu wakiwemo wanasiasa mbalimbali wanaokebehi jitihada zake anazozifanya za maendeleo, alisema watu hao wanapaswa kupuuzwa.

“Wapuuzeni maana wengine wanalipwa lipwa visenti ili waje kututukana. Watu kama hao wahakosi…hao wapo wapuuzeni,” alisema.

 MAOFISA  waliokwenda Canada kuipokea ndege ya pili ya Airbus A220-300 wakilakiwa kwa shangwe Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.


Hata hivyo, Magufuli,  aliwataka Watanzania kwa ujumla wao wapendane na kushikamana kuijenga nchi yao na kwamba vyama vya siasa visiwafanye kuleta uchonganishi.

“Vyama vya siasa vitusifanye tulumbane. Umoja wetu ni muhimu sana. Maendeleo yaliyopatikana ndani ya miaka mitatu ni  rasha rasha tu mvua zenenyewe zinakuja.

“Wachonganishi wakashindwe na kulegea kwa majina yote ya Yesu na Mohamad ili tuwe na maendeleo,” alisema Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli, aliwapongeza Watanzania wote kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake ikiwemo kununua ndege 7 zilizowezesha kuimarishwa kwa ATCL.

Pia kwa kutekelezwa kwa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) na mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji, na kwamba kwa mwendo huu mambo mengine mengi makubwa yanakuja.


 DK. Magufuli, akipungia wananchi baada ya kupokea ndege ya pili ya Airbus A220-300.


Magufuli pia, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi na wafanyakazi wote wa ATCL kwa kazi nzuri wanayofanya wakiwemo Marubani vijana wa Kitanzania watatu walioendesha ndege hiyo kutoka Montreal nchini Canada hadi Jijini Dar es Salaam Tanzania, na amebainisha kuwa hayo ni matunda ya kununua ndege mpya na kuimarisha ATCL.

“Tumeambiwa hapa tangu tuanze kununua ndege hizi ATCL imeongeza idadi ya Marubani kutoka 11 hadi 50, walioajiriwa ni vijana wetu wa Kitanzania, na kwa ujumla wafanyakazi wapya wa ATCL walioajiriwa ni 380, hivi kama tusingenunua ndege hizi vijana hawa wangeendesha nini? Wangeendesha matoroli? Lakini sasa wamepata ajira wananufaika wao na familia zao au jamaa zao” alisema Magufuli.

Alisisitiza kuwa ndege hizi zote zimenunuliwa kwa fedha za Watanzania kwa asilimia 100, na amewataka Watanzania wote kuelewa kuwa maendeleo ya Tanzania yataletwa na Watanzania wenyewe na kwamba hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea kwa kutegemea misaada.

“Tunahitaji misaada lakini iwe ni misaada ya kutuwezesha kusonga mbele kimaendeleo na kujitegemea na sio kutulemaza, sekta binafsi pia tunaihitaji, lakini iwe ni sekta binafsi ya manufaa kwa Taifa.

“Hata leo (jana) amekuja Mwenyekiti wa Bharti Airtel, tumezungumza na amekubali kuongeza hisa za Serikali katika airtel kutoka 40 hadi 49 na kupunguza hisa kwenye kampuni yake kutoka asilimia 60 hadi 51 bila kutudai malipo yoyote, pia Airtel itatoa gawio kwa Serikali wakati miaka minane yote ya nyuma haikuwahi kutoa hata senti tano,” alisema Magufuli.

Aidha, Magufuli,  ameagiza ndege mbili za Serikali (Fokker 28 na Fokker 50) zilizokuwa zikitumiwa kusafirisha viongozi zipigwe rangi za ATCL na kuanza kusafirisha abiria ili kuiongezea uwezo ATCL na kuwawezesha Watanzania wote kupata huduma za usafiri wa anga.

 RAIS Dk. John Magufuli, akiwa na viongozi mbalimbali akikata utepe kuashiria kupokea ndege mpya ya pili ya Airbus A220-300 iliyowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam jana Januari 11, 2019. (Picha zote na Ikulu).

Mapema Naibu Spika, Tulia Ackson, aliipongeza Serikali kwa juhudi kubwa za kuimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege mpya, na amefafanua kuwa anafurahi kuona matunda ya fedha zinazopitishwa na Bunge katika bajeti.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alimshukuru Rais Magufuli, kwa kuongoza juhudi za kuleta mageuzi ya kiuchumi hapa nchini na amemhakikishia kuwa Watanzania wanamuunga mkono na wapo tayari kuhakikisha nchi yao inasonga mbele.

No comments