Breaking News

SERIKALI MTANDAO YARAHISISHA UPATIKANAJI WA HUDUMA KWA WANANCHI KWA WAKATI

Utekelezaji wa Serikali Mtandao ni moja ya sehemu muhimu ya maboresho yaliyofanyika katika utumishi wa umma, ambao umesaidia kurahisisha utoaji wa huduma katika taasisi za umma zinazopatikana kwa urahisi, kwa wakati na kwa gharama nafuu kwa kutumia TEHAMA.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakati akifungua kikao kazi cha pili cha Serikali Mtandao chenye lengo la kuwakutanisha wadau wanaohusika na utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa ajili ya kujenga uwezo, kuongeza ushirikiano na kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na kujadiliana njia sahihi za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Serikali Mtandao.

Bw. Kiliba amefafanua kuwa, utekelezaji wa Serikali Mtandao, umechangia kwa kiasi kikubwa katika kurahisisha utoaji wa taarifa na huduma nyingine kwa wananchi kwa haraka, uwazi, gharama nafuu wakati wowote na kuongeza kuwa, Serikali Mtandao ni kichocheo muhimu katika kufikia Dira ya Taifa ya Mwaka 2025 inayolenga pamoja na mambo mengine, kufikia maendeleo ya viwanda. 

Bw. Kiliba ameongeza kuwa, utekelezaji wa Serikali Mtandao umejikita katika kuboresha utoaji wa huduma miongoni mwa taasisi za umma, kati ya taasisi za umma na wananchi, kati ya taasisi za umma na sekta ya biashara na kwa serikali kuwahudumia watumishi.

Bw. Kiliba ameainisha kuwa, utekelezaji wa Serikali Mtandao unalenga kuimarisha utawala bora na kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi za umma kwa kuhakikisha uwepo wa mawasiliano ya haraka, yenye uhakika na salama ndani na kati ya taasisi mbalimbali za serikali. 

Aidha, Bw. Kiliba ametoa wito kwa washiriki kuelekeza majadiliano katika kauli mbiu ya kikao kazi hicho inayosema “Uwianishaji wa Rasilimali za TEHAMA kwa Maendeleo ya Viwanda” ambayo imelenga kuonyesha umuhimu na nafasi ya TEHAMA katika maendeleo ya viwanda nchini.

Bw. Kiliba amesisitiza kuwa, kauli mbiu hiyo inatukumbusha kwamba ukuaji wa viwanda nchini unategemea pamoja na mambo mengine, uwezeshaji wa TEHAMA, ambao unasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuwezesha kufanya maamuzi sahihi na kwa haraka ikiwa ni pamoja na wananchi kupata huduma mbalimbali kama vile uanzishaji wa biashara na uombaji wa vibali mbalimbali.

Kikao kazi hiki cha pili cha kundi la kwanza kinahudhuriwa na Maofisa TEHAMA, Maofisa Ununuzi, Maofisa Mawasiliano Serikalini, Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala, Wakaguzi, Wahandisi, Wahasibu, Maofisa Mipango na watumiaji wa mifumo ya TEHAMA.


IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
 TAREHE 30 JANUARI, 2019
 Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba akifungua rasmi kikao kazi cha Serikali Mtandao kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu Dodoma mapema
Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wakala ya Serikali Mtandao pamoja na washiriki wa kikao kazi cha Serikali Mtandao mara baada ya kufungua rasmi kikao kazi cha Serikali Mtandao kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu Dodoma mapema leo
 Baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Serikali Mtandao wakimsikiliza Mkurugenzi Idara ya Ushauri na Uchambuzi Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu Dodoma mapema
 Mkurugenzi Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Priscus Kiwango akitoa neno la shukrani na kuahidi kutekeleza maelekezo ya mgeni rasmi baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha Serikali Mtandao katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano uliopo Chuo Kikuu Dodoma mapema leo.

No comments