Breaking News

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU WAAJIRI KUHAMISHA MTUMISHI AKIWA NA KESI KAZINI *WATAKAOSHINDWA KUWASILISHA VIELELEZO VYA RUFAA ZILIZOKATWA NA WATUMISHI WA UMMA KUKIONA.


NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma, mara baada ya kumalizika kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi  wa Tume hiyo cha kuhimiza uwajibikaji  kilichofanyika Makao Makuu ya Tume hiyo Ubungo Plaza Jijini Dar es Salaam jana Januari 16, 2019. (Picha zote na James Mwanamyoto-UTUMISHI).

                           
                                Na Mary MwakapedaWAJIRI na Mamlaka za Ajira Nchini watakaoshindwa kuwasilisha vielelezo vya rufaa zilizokatwa na watumishi wa umma  kwenye Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 14 kama sheria inavyoelekeza, watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuikwamisha tume hiyo kutekeleza jukumu lake la kushughulikia kwa wakati rufaa hizo.

Kauli hiyo imetolewa jana Januari 16, 2019 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa.

Naibu Waziri Mary, alikuwa akizungumza na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma  Makao Makuu ya Tume hiyo, akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya Tume na kujiridhisha namna Tume  hiyo inavyotekeleza majukumu yake.

 KAIMU Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Richard Odongo, akieleza majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Naibu Waziri Dk. Mary.Alisema, kitendo cha waajiri hao kutowasilisha vielelezo vinavyohitajika na Tume ya Utumishi wa Umma kwa wakati ili kuiwezesha tume kufanya maamuzi sahihi ya rufaa,  imekuwa ni kikwazo cha utekelezaji wa majukumu yake kama vile kusimamia, kufuatilia na kutathmini uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma Nchini.

Dk. Mary, alisisitiza kuwa Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma  kuhakikisha inatoa elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa kufanyia kazi rufaa zinazowasilishwa ili waweze kujua ni muda gani unaotumika kushughulikia rufaa zao, na kuongeza kuwa elimu hiyo itapunguza malalamiko dhidi ya tume kuwa haifanyii kazi rufaa zao kwa wakati.

Aidha, alisema kuwa, kuanzia sasa ni marufuku kwa mwajiri yeyote kumhamisha mtumishi aliyebainika kuwa na kosa  mahala pa kazi kwasababu Tume ya Utumishi wa Umma itashidwa kushughulikia suala la mtumishi huyo na kuna uwezekano mkubwa akafanya tena makosa yale yale anakohamia.

 BAADHI watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri Mary (hayupo pichani).Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Richard Odongo alisema kuwa, majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma yameainishwa katika Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298  Kifungu 10 (1) ambapo imepewa mamlaka ya kutoa miongozo na kuhakikisha Utumishi wa Umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

Odongo alisema, Tume ya Utumishi wa Umma ni Mamlaka ya Rufaa kwani inapokea na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma, hivyo inafanya kazi kama mahakama ndani ya Utumishi wa Umma na ni chombo cha kutoa haki kwa watumishi wanaoonewa na inasimama kama mdhamini kuhakikisha haki inatendeka pande zote yaani kwa mwajiri na mtumishi.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu, Dkt. Steven Bwana, amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi aliyoyatoa na kuahidi kusimamia utekelezaji wake.

 MWENYEKITI wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu, Dk. Steven Bwana, akifafanua majukumu ya bodi yake.Tume ya Utumishi wa Umma iliundwa kwa Mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 ili kuhakikisha kuwa, Utumishi wa Umma unakuwa mmoja na watumishi wote wanakuwa na taratibu za usimamizi, hadhi, haki na masilahi yanayofanana.

No comments