SERIKALI YATOA BILIONI 2.5 KWA AJILI YA UJENZI WA JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Ummy Mwalimu, akzungumza wagonjwa katika Kituo cha
Afya cha Kambarage mjini Shinyanga jana Januari 24, 2019.
NA WAMJW-SHINYANGA
SESRIKALI kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa kiasi cha sh. Bilioni 2.5 zitakazotumika
katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa
wa Shinyanga, lengo likiwa ni kutoa huduma za kibingwa kwa akina mama
wajawazito na watoto wachanga.
Hayo yalisemwa jana Januari 24, 2019
na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu,
wakati alipotembelea ujenzi wa Hospitali hiyo na kukuta jengo la wagonjwa wa
nje (OPD) na Utawala likiwa limekamilika.
Waziri Ummy, alisema fedha hizo
zitafika katika hospitali hiyo ndani ya wiki mbili ili ziweze kuchochea kasi ya
ujenzi na lengo ifikapo mwezi Septemba 2019 ianze kutoa huduma za afya.
“Ninaahidi kutoa sh. Bilioni 2.5
ndani ya wiki mbili ziweze kutumika katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto,
lengo la serikali ni kuhakikisha kila mama mjamzito anapofika hospitalini
kujifungua atoke akiwa salama yeye na kichanga chake,” alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy, amefikia uamuzi huo
baada ya kupokea ripoti ya mkoa kuhusu vifo vitokanavyo na uzazi kutoka kwa
Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Mfaume Rashid, ambapo kwa mwaka 2016/2017 kulikua na
vifo 73, na mwaka 2017/2018 vikiwa ni vifo 56, hali ambayo Waziri huyo
ameonekana kutoridhishwa nayo.
Hata hivyo, Waziri Ummy aliahidi
kuongeza fedha zingine kiasi cha shilingi bilioni 3 ndani ya mwezi mmoja,
zitakazotumika katika ujenzi wa jengo kwa ajili ya huduma za uchunguzi ikiwemo
huduma za maabara, X-ray na CT-Scan pia jengo hilo litakua na vyumba vitatu vya
upasuaji.
Waziri Ummy, alisisitiza ujenzi wa
jengo hilo utumike wa mfumo wa Force Account ambao utahakikisha wananchi
wanashiriki kwa asilimia 100 katika kufanikisha ujenzi huo na huduma za afya
zianze kutolewa mapema.
Wakati huo huo, Waziri Ummy,
ametembelea kituo cha afya cha Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga
kuona hali ya miundombinu ya kituo hicho na utoaji wa huduma za afya huku kwa
kiasi kikubwa akionekana kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa majengo ya huduma
mbalimbali.
Kuhusu uhaba wa watumishi wa kada za
afya waziri huyo ameahidi kutatua changamoto hiyo hali inayopelekea kuwepo kwa
msongamano wa wagonjwa.
Waziri Ummy amehitimisha ziara yake
katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Shinyanga na kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na hali ya utoaji wa huduma za afya
hasa katika jengo la huduma za mama na mtoto na pia katika jengo la kuhifadhia
watoto wachanga wenye uhitaji wa uangalizi maalumu (NICU).
UMMY, akipanda mti wa kumbukumbu katika kituo cha Afya
cha Kambarage kilichopo katika Manispaa ya Shinyanga.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akikagua jengo la wagonjwa wa nje (OPD)
ambalo limekamilika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneka na kulia ni Katibu Tawala wa
Mkoa huo Albert Msosela.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Ummy Mwalimu, akimjulia hali mtoto mchanga aliyezaliwa katika Kituo cha
Afya cha Kambarage mjini Shinyanga.
WAZIRI Ummy, akioneshwa ramani ya
majengo ya Kituo cha Afya cha Kambarage na Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Lusajo
Mwakajoko, wakati alipotembelea kituo hicho jana kilichopo manispaa ya
Shinyanga.
UMMY, akiangalia kichanga kilicholazwa katika
chumba maalumu cha uangalizi wa watoto mahututi na wale waliozaliwa kabla ya
siku (njiti) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Kushoto ni Daktari
Bingwa wa watoto Dk. Mwita Ngutunyi.
No comments