Breaking News

TANESCO YAPEWA SIKU TATU KUUNGANISHIA UMEME WIZARA 10 DODOMA.
https://mail.google.com/mail/u/0/images/cleardot.gif

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kaleman (Kati kati), akikagua ujenzi wa jengo la Wizara hiyo unaondelea sasa katika Mji wa Serikali Ihumwa Jijini Dodoma leo Januari 7, 2019.

                 Na Teresia Mhagama, Dodoma

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuunganisha  umeme katika wizara kumi ambazo bado hazijalipia gharama ya kuunganishiwa umeme katika maeneo yao ya ujenzi kwenye Mji wa Serikali uliopo Ihumwa Jijini Dodoma. 

Alitoa agizo hilo leo Januari 7, 2019 Jijini Dodoma baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme na ujenzi wa majengo ya Serikali katika eneo hilo la Ihumwa ambapo aliambatana Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Hamisi Mwinyimvua.

Baadhi ya viongozi wengine alioambatana nao ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga.


KALEMANI (mwenye shati la bluu), akizungumza na wafanyakazi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaofanya kazi ya kuunganisha umeme katika Mji wa Serikali, Ihumwa Jijini Dodoma.

Dk. Kalemani, alisema kuwa, Serikali imetoa Transfoma kwa ajili ya kufungwa katika maeneo ya wizara zote 22 kwenye Mji wa Serikali ili kazi za ujenzi zifanyike usiku na mchana na hivyo kuwezesha ujenzi wa majengo kukamilika mwisho wa mwezi huu kama ilivyopangwa.

“Tumeshatoa transfoma, na tunatarajia zifanye kazi, hivyo nimewaelekeza wataalam wangu kuwa pamoja na kwamba hizo wizara hazijalipia gharama, transfoma zifungwe katika maeneo yao ndani ya siku tatu na wizara hizo zianze  kutumia umeme huo ndani ya siku tano kwani malipo ni 921,000 tu,” amesema Dk. Kalemani.

Alieleza kuwa,  jumla ya wizara kumi ambazo tayari zimeshalipia umeme, Tanesco wanafanya kazi ya kuunganisha  nishati hiyo, ndani ya siku mbili.


 KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Hamisi Mwinyimvua, (katikati), Kaimu Kamishna wa Umeme na  Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kushoto) na  Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo (wa kwanza kulia), wakikagua kazi ya usambazaji umeme katika Mji wa Serikali, Ihumwa,  Jijini Dodoma.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati,  amemuagiza mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuongeza kasi ya ujenzi ili jengo hilo liwe limekamilika ifikapo tarehe 30 mwezi huu.

Aidha, alieleza  kuwa, atakuwa akikagua kazi ya ujenzi wa jengo kila baada ya siku tano ili kuona kama linaenda kwa kasi na ubora  kwa kuwa  mkandarasi huyo amekwilipwa fedha.

No comments