Breaking News

TANZANIA KUNUFAIKA ZAIDI NA MAKUBALIANO MAPYA NA KAMPUNI YA SIMU ZA MKONONI YA BHARTI AIRTEL.


                             RAIS DK. JOHN MAGUFULI
 
                                      Na Mwandishi Wetu

RAIS John Magufuli, jana Januari 15, 2019 ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Bharti Airtel ya India juu ya umiliki wa hisa za Kampuni Airtel Tanzania na maslahi mengine ya Tanzania kutokana na biashara ya kampuni hiyo.

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi alitia saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mwenyekiti wa Bharti Airtel Sunil Mittal, alitia saini kwa niaba ya Kampuni ya Bharti Aitel.

Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi alisema katika makubaliano hayo Kampuni ya Bharti Airtel imekubali kupunguza umiliki wa hisa zake za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 60 hadi 51 na hivyo kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 bila malipo yoyote kutoka Serikalini.

Prof. Kabudi, alibainisha maeneo mengine ya makubaliano kuwa ni Serikali kupata gawio la kila mwaka kutokana na umiliki wake wa asilimia 49 ambapo inakadiriwa itakuwa ikipata sh. Bilioni 10, kufutwa kwa madeni yote ya kampuni ya Airtel yaliyokuwa yamefikia sh. Trilioni 1, Bharti Airtel itatoa sh. Bilioni 1 kila mwezi kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia Aprili 2019 ili kuonyesha nia njema, pia kampuni hiyo itatoa sh. Bilioni 2.3 kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii.

Maeneo mengine ya makubaliano ni Bodi ya Wakurugenzi wa Airtel Tanzania kuundwa na wajumbe 7 ambapo Serikali ya Tanzania itawakilishwa na wajumbe 3 (akiwemo Mwenyekiti atakayeteuliwa na Serikali) na Bharti Airtel itawakilishwa na wajumbe 4, Menejimenti ya Airtel Tanzania itaongozwa na Bharti Airtel, lakini Ofisa Mkuu wa Ufundi atateuliwa na Serikali ya Tanzania.

Pande zote mbili zitashirikiana kuandaa upya nyaraka muhimu za kusaidia uendeshaji wa kampuni, pande zote mbili zitashirikiana kuongeza tija na ufanisi wa Airtel Tanzania na pande zote mbili zitashirikiana kutumia miundombinu ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ikiwa kuna hoja za kibiashara.

Kwa upande wake Sunil Mittal, alisema amefurahishwa na kufikiwa kwa makubaliano katika mazungumzo hayo na amebainisha kuwa awali aliona kuna ugumu wa kufikia makubaliano, lakini baadaye alielewa kuwa lengo la Rais Magufuli, ni kuhakikisha anaweka mwelekeo mzuri wenye manufaa kwa Tanzania.

Mittal aliongeza kuwa makubaliano hayo yameandika historia mpya kwa hisa nyingi kumilikiwa na Watanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania na kwamba anatarajia kuwa Airtel Tanzania itaendelea kufanya vizuri katika soko la Tanzania ambayo ni nchi yenye uwekezaji mkubwa wa Bharti Airtel Barani Afrika.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini makubaliano hayo Rais Magufuli aliipongeza timu iliyoiwakilisha Serikali ya Tanzania chini ya Prof. Kabudi na timu ya Mittal kwa kufikia makubaliano hayo yaliyochukua muda wa miezi 8 na ameelezea furaha yake kuwa sasa Airtel Tanzania itaanza kutoa manufaa kwa Serikali ikiwemo gawio na maslahi mengine yanayostahili, mambo ambayo hayakufanyika kwa miaka zaidi ya 8 tangu kampuni hiyo ianzishwe hapa nchini.

Alimpongeza Mittal kwa kuridhia kuongeza hisa za Serikali, kutoa sh. Bilioni 1 kila mwezi kwa miaka 5 na kutoa mchango wa Sh. Bilioni 2.3 ambazo ameagiza ziungane na sh. Bilioni 1 iliyotengwa kwa ajili ya sherehe za siku ya Uhuru za mwaka 2018 na kufanya jumla sh. Bilioni 3.3 kwenda kujenga hospitali katika makao makuu ya nchi Jijini Dodoma.

“Huu ndio uwekezaji ninaoutaka, uwekezaji ambao tuna faida nao, Airtel ilikuwepo tangu miaka 8, 9 iliyopita lakini tulikuwa hatupati kitu, sasa tutapata fedha, na hili liwe somo kwetu Watanzania wote kuwa Serikali inapotetea maslahi ya Watanzania haizungumzi kutoka hewani, tujifunze kuwaheshimu watalaamu wetu,” alisisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli alimhakikishia Mittal na wawekezaji wote hapa nchini kuwa Tanzania ni nchi nzuri ya kuwekeza na itadumisha utamaduni wa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kutambua kuwa uwekezaji huo unasaidia kuzalisha ajira na kuiwezesha Serikali kupata mapato.

No comments