Breaking News

TUCTA LATOA ONYO KALI KWA WANASIASA WANAOTAFUTA UMAARUFU KUPITIA MGONGO WAKE * WAZIRI MKUU APOKEA MAANDAMANO YA WAFANYAKAZI WAKIMPONGEZA MAGUFULI.






WATUMISHI wa Ofisi ya Bunge, wakipita mbele ya mgeni rasmi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, katika maandamano ya amani ya vyama vya wafanyakazi, yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma,  leo Januari 7, 2019. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)



                       Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) limeyataka makundi ya wanasiasa kutowatumia wao kama njia ya kujitafutia umaarufu kwa kuzungumzia masuala yao na badala yake wawaachie viongozi wa vyama hivyo kwa sababu wanajitosheleza.

Pia shirikisho hilo limesema litaendelea kuiunga mkono na kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano pamoja na Rais wake Dk. John Magufuli na kwamba watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya ajira zao.
  WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, akishiriki kuimba wimbo wa mshikamano wa wafanyakazi maarufu kama "Solidarity Forever" kwenye maandamano ya amani ya vyama vya wafanyakazi,

Hayo yamesemwa leo Januari 7, 2019 na Katibu Mkuu wa TUCTA, Yahya Msigwa, katika hotuba yake aliyoitoa kwa wafanyakazi baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kupokea maandamano ya amani ya vyama vya wafanyakazi.

Watumishi wa taasisi mbalimbali leo wameandamana Jijini Dodoma katika viwanja vya Nyerere Squarekwa lengo la kumpongeza Rais Dk. Magufuli, kwa uamuzi wake kufuta kikotoo kipya cha mafao ya wafanyakazi kilichopendekezwa katika kanuni za sheria ya Mifuko ya Jamii.

 MAKAMU wa Rais TUCTA Qambos Sule, akizungumza mbele ya watumishi katika maandamano ya amani ya vyama vya wafanyakazi kwenye viwanja vya Nyerere Square.

Katibu huyo wa TUCTA alisema mara nyingine makundi ya wanasiasa yamekuwa yakisema maneno ambayo wao hawajayasema jambo ambalo limekuwa likiwachonganisha na wadau wao wakiwemo wanachama pamoja na Serikali.

”Wafanyakazi wanaona fahari kwa sababu Rais Dk. Magufuli, anasikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kuzitatua kwa wakati. Aliposema atafufua Shirika la Ndege Tanzanzia amelifufua na sasa tuna ndege saba pamoja na ujenzi wa miradi mkubwa ya umeme, barabara ambayo yote inaenda kutengeneza ajira,” alisema.
 KATIBU Mkuu wa TUCTA Dk. Yahya Msigwa, akizungumza mbele ya watumishi katika maandamano ya amani ya vyama vya wafanyakazi kwenye viwanja vya Nyerere Square.

Hata hivyo, ameiomba Serikali ifanye uchunguzi kwenye miradi inayotekelezwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa sababu hawana uhakika kama miradi hiyo imerejesha fedha.

Pia ameiomba Serikali iongeze mishahara kwa watumishi wa umma.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema Serikali ipo tayari wakati wote kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuboresha mishahara na maslahi yao.

 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akizungumza kwenye maandamano ya amani ya vyama vya wafanyakazi katika viwanja vya Nyerere Square.



“Wito wa Serikali ni kuwa wafanyakazi watekeleze majukumu yao kwa uadilifu,weledi na kujituma ikiwa ndio chachu ya kufikia malengo na ustawi wa nchi yetu,” alisema Majaliwa.

Kuhusu suala la kupandisha mishahara, madaraja  na maslahi ya wafanyakazi kwa ujumla, Waziri Mkuu alisema  Rais Dk. Magufuli, alishalitolea maelekezo na kwamba Serikali inayafanyia kazi maelekezo yake, hivyo amewaomba wafanyakazi waendelee kuwa wavumilivu.


 BAADHI ya viongozi washiriki katika maandamano hayo.

Alisema, Serikali imeendelea kulipa stahili za watumishi wa umma kwa wakati  na kulipa madeni hatua kwa hatua, ambapo kati ya Julai 2018 hadi Septemba 2018, Serikali imelipa sh. Bilioni 184.9 za madai mbalimbali ya watumishi.

“Kati ya kiasi hicho Serikali imelipa sh. Bilioni 49 kwa ajili ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 28,214 ambayo yanajumuisha sh. Bilioni 19.2 walizolipwa walimu 16,214. 
 

 WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, akihutubia watumishi walioshiriki maandamano hayo ya amani leo Januari 7, 2019 Jijini Dodoma.

Aliaema hata hivyo, Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi katika wizara na taasisi mbalimbali ili kupanga vizuri mishahara na motisha kwa watumishi wa umma.

No comments