Breaking News

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KUUNGANISHIWA UMEME WA UHAKIKA NCHI NZIMA- KALEMANI.


WAZIRI wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Chato, Dk. Medard Kalemani, (kushoto) na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, wakifungua kitambaa maalumu kuashiria uwekaji jiwe la msingi la Kiwanda cha Uchenjuaji Dhahabu cha Padalu, kilichopo Chato Geita, jana Januari 2, 2019.

                         Na Veronica Simba, Geita

WIZARA  ya Nishati inatekeleza mkakati wa kuwaunganishia umeme wa uhakika wachimbaji wadogo wa madini kote nchini, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais John Magufulu kuiwezesha sekta hiyo izalishe kwa tija kwa manufaa yao binafsi na ya Taifa kwa ujumla.

Akizungumza jana Januari 2, 2019 katika hafla ya kuweka jiwe la msingi wa kiwanda cha kuchenjua dhahabu kinachomilikiwa na kampuni ya Padalu, Kijijini Lumasa, Chato, Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani, alisema serikali imefunga Transfoma tano zenye uwezo wa KVA 400 hadi 1,000 ili kuwawezesha wachimbaji wadogo wa Geita kuzalisha kwa tija.
MSIMAMIZI wa Kiwanda cha kuchakata Dhahabu cha Padalu, kilichopo Chato Geita, Abel Lucas (kulia), akitoa maelezo jinsi kinavyofanya kazi kwa Waziri wa Nishati Dk. Kalemani pamoja na Naibu Waziri wa Madini Biteko na ujumbe waliofuatana nao, wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi wa kiwanda hicho.

“Umeme huu mkubwa utawawezesha wachimbaji kuchimba , kuchenjua na kuongeza thamani dhahabu yao ili kuiongezea thamani, iwapatie faida na waweze kulipa kodi na mrabaha serikalini,” alisema.

Alisema, yako maeneo mkoani humo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo lakini akabainisha kuwa utaratibu wa kufunga transfoma nyingine tano zenye uwezo uleule unafanyika ili kuyafikia maeneo ya wachimbaji yaliyosalia ikiwemo Mbogwe na Nyakafuru.
MSIMmizi wa kiwanda hicho Lucas (kushoto), akitoa ufafanuzi zaidi wa matumizi ya kiwanda hicho kwa Dk. Kalemani.

Aidha, alifafanua kuwa umeme uliounganishwa kwa ajili ya kiwanda hicho cha kuchenjua dhahabu, utawanufaisha pia wananchi wa maeneo jirani ambao wataanza kuunganishiwa huduma hiyo kuanzia wiki ijayo.

Pia, Kalemani alitumia fursa hiyo kufafanua kuhusu gharama za umeme katika maeneo ya vijijini ambapo alibainisha kuwa serikali imedhamiria wananchi wa vijijini watozwe shilingi 27,000 tu kwa ajili ya huduma ya kuunganishiwa umeme.

“Wananchi maeneo yote ya vijijini nchi nzima, gharama za kuunganishiwa umeme ni sh. 27,000 tu. Msikubali kutozwa zaidi. Iwe ni umeme wa REA au wa TANESCO, gharama ni hiyo hiyo na siyo zaidi,” alisisitiza Waziri Kalemani.
BAADHI ya wananchi walioshiriki katika hafla hiyo wakimsikiliza Waziri Dk. Kalemani, (hayupo pichani).

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alipongeza jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Wizara ya Nishati katika kuhakikisha wachimbaji madini wadogo nchini wanakuwa na uchimbaji wenye tija kwa kuwapelekea huduma ya umeme.

Awali, uongozi wa kiwanda hicho cha uchenjuaji dhahabu ulieleza kuwa ujenzi wake ulifanyika kufuatia agizo la Rais Magufuli la kuwataka wachimbaji kuyaongeza thamani madini yao hapa nchini kabla ya kusafirisha nje ya nchi.

No comments