Breaking News

WAZANZIBARI WAPUUZENI WANAOBEZA MAENDELEO YA ELIMU YETU-BALOZI IDDI 

MAKAMU wa  Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la Shule  ya Sekondari ya Uweleni Mkoa wa Kusini Pemba leo Januari 8 , 2019.

                                    Na Othman Khamis Ame, Zanzibar
 

IMEELEZWA kuwa Wazanzibar  wana kila sababu ya kujivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika Sekta ya Elimu yaliyosimamiwa na Chama cha Afro Shirazy Party  na Baadae CCM katika kipindi chote cha  miaka 55 toka kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyouondoa Utawala wa Kibaguzi katika Elimu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi Seif Ali Iddi,  aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Shule ya Sekondari ya Uweleni iliopo Mkoani Kisiwani  Pemba katika shamra shamra za kusherehekea miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  ya mwaka 1964.


 WANAFUNZI  wa Shule ya Sekondari ya Uweleni wakishangiria kumpokea mgeni rasmi Balozi Iddi.Balozi Iddi,  alisema hatua iliyofikia Taifa hivi sasa katika Sekta ya Elimu ni kubwa kiasi kwamba wale wanaokebehi wanashindwa kujifahamu kwamba wanajidharau wao wenyewe  na dawa yao ni kupuuzwa kwa sababu hawajui thamani ya kuwa na chao na wala sio watu wanaothamini cha wenzao.

Alisema tokea wananchi wa Zanzibar walipojitawala  kutoka katika makucha ya kibeberu, vijana wa visiwa hivi sasa wanaendelea kupata elimu bila ya malipo, kuanzia maandalizi yasekondari ambapo pia wakifikia vyuo vikuu kuna utaratibu wa kuwapatia udhamini kwa wale wanaofanya vizuri.

 SURA ya jengo jipya linalojengwa katika  eneo la Shule  ya Sekondari ya Uweleni Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.BaloziIddi  alieleza kwamba miongoni mwa mambo yaliyoahidiwa na Chama cha Afro Shirazy Party wakati wa kupigania Uhuru kwamba iwapo chama hicho kitashika hatamu elimu kwa watoto wa wakulima na wafanyakazi itatolewa bure bila ya malipo.

Alifahamisha kwamba historia inaonyesha wazi kuwa kabla ya ukombozi shule za sekondari zilikuwa kidogo akatolea mfano kisiwani Pemba ilikuwepo moja tu ya Fidel Castro, ikimaanisha kwamba Wilaya nzima ya Mkoani wakati huo haikuwa na shule ya sekondari.

 BAADHI ya wanafunzi wa shule hiyo walifuatilia kwa makini  hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi.Makamu wa Pili  alisema uwepo wa jengo hilo utarahisisha upatikanaji wa taaluma ambayo itawaandaa vijana mbali ya kuwa wataalamu wa taasisi za umma hapo baadae lakini pia watajiepusha na mambo yanayoweza kuwaletea madhara.

Balozi Iddi aliipongeza umoja ulitumika katika ujenzi wa jengo la shule hiyo ikiwa ni ushahidi tosha utakaowafanya walengwa wake kushiriki kikamilifu kuhimiza malengo ya kitaaluma na kimaadili yaliyokusudiwa.

 MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpongeza Ustaadhi Khamis Ali wa Wilaya ya Mkoani baada ya kusoma Quran kwenye hafla hiyo.Akitoa taarifa ya kitaalamu ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa ,  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,  Abdullah Mzee Abdullah,  alisema ujenzi huo umetokana na uhaba ya madarsa sambamba na kuzingatia Sera ya Elimu ya ujenzi wa shule za ghorofa kwa lengo la uhifadhi ya ardhi ndogo iliyopo.

Abdulah alisema inapendeza kuona wananchi mbali mbali hasa wale wenye wakijitolea nguvu zao zilizowezesha maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo kwenda kwa kasi kubwa.


 NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mheshimiwa Mmanga Mjengo Mjawiri akitoa ufafanuzi wa takwimu za ongezeko la Shule Nchini kabla na baada ya Mapinduzi.


Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeamua kujenga majengo makubwa ya ghorofa ili kila mtoto wa Visiwa Vya Unguja na Pemba waliotokana na mifupa ya wakwezi na wakulima wanapata haki yao ya  elimu.

Naibu katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar alisisitiza kwamba ongezeko la shule za sekondari nchini hivi sasa linatia moyo na kuleta faraja kwa Jamii kutoka shule 4 za sekondari kabla ya Mapinduzi na kufikia  204 za sasa Unguja na Pemba.

Takwimu hiyo inaonyesha wazi kwamba Kisiwa cha Unguja hivi sasa kina shule 124 za sekondari wakati Kisiwani cha Pemba kimefanikiwa kuwa na 80 kiwango kinachoonyesha wastani wa shule 10 za sekondari kwa kila Wilaya ya Zanzibar.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mmanga Mjengo Mjawiri alisema Zanzibar hivi sasa ina shule 202 za msingi kutoka moja kabla ya Mapinduzi mwaka 1964.


 BALOZI Iddi akizungumza na Wananchi wa Pemba  baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo jipya la Shule ya Sekondari ya Uweleni Pemba.

Picha na – OMPR – ZNZ.Mmanga alisema mfumo wa elimu Zanzibar hivi sasa umeimarika vyema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi  zaidi ya elfu 9,000 kwenye vyuo vikuu vya Zanzibar  pekee.

Alisema ufaulu wa wanafunzi hivi sasa umefikia asilimia 98% katika kiwango cha sekondari kinachowawezesha kuwa na sifa za kujiunga na vyuo Vikuu mbali mbali.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshatenga sh. Bilioni 2 kwa ajili ya ununuzi wa madaftari mengine ya vipindi vijavyo na mchakato wa ununuzi huo unaendelea.

No comments