Breaking News

WAZIRI MKUU APOKEA LESENI YA USAJILI WA TANZANIA SAFARI CHANEL.

 WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza  na wajumbe wa Kamati Maalumu iliyoundwa na Serikali ya kusimamia uboreshaji wa Channel ya Utalii ya  TBC ya Tanzania Safari Channel, Ofisini kwake, Mlimwa, Jjijini Dodoma jana Januari 16, 2019. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).


                                 Na Irene Bwire, Dodoma

 WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amepokea Leseni ya usajili wa chaneli ya utalii ya Tanzania Safari ambayo itaiwezesha kuonyeshwa kwa umma bila ya malipo yoyote (Must-carry Channel) na wamiliki wa visimbusi.

Waziri Mkuu amekabidhiwa Leseni hiyo jana Januari 16, 2019 kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa, Jijini Dodoma ambako alitaka apewe mrejesho kutoka kwa wajumbe wa Kamati Maalumu ya kusimamia uboreshaji wa Chaneli ya Utalii (Tanzania Safari Channel).MAJALIWA, akimshukuru Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji),  Doroth Mwaluko, wakati alipokabidhiwa Hati ya Usajili wa Channel ya Utalii ya TBC ya  Tanzania Safari Channel  katika kikao cha kuboresha channel hiyo alichokiitisha, Ofisini kwake Jijini Dodoma. Wapili kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC),  William Kallaghe na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Ayoub Ryoba.


Akikabidhi Leseni hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk. Ayoub Rioba, alisema kukamilika kwa usajili huo kumeiwezesha chaneli hiyo ianze kuonekana kwenye kisimbusi cha AZAM namba 109.

Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Dk. Rioba amesema, kamati hiyo iliundwa Desemba 21, 2018 na inajumuisha wajumbe kutoka taasisi ambata za maliasili na utalii kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

 WAZIRI  Mkuu Majaliwa, akionyesha  Cheti cha Usajili wa Channel ya Utalii ya Shirika la Utangazaji Tanzania  (TBC) ya Tanzania Safari  Channel baada ya kuzungumza na Kamati  Maalumu iliyoundwa na Serikali ya Uboreshaji wa  Channel hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Ryoba.
“Baada ya kupata leseni, sasa hivi tunaonekana kwenye kisimbusi cha AZAM chaneli namba 109 na pia kwenye Intelsat ambako tutaweza kuonekana kwenye nchi zote Barani Afrika, sehemu kubwa ya Bara la Ulaya na Uarabuni,” alisema.

Mapema, akichangia hoja kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali (Mst.) Hamisi Semfuko alisema, chaneli hiyo inaweza kunufaika kwa kupata matangazo kutoka kwa wamiliki wa hoteli, kampuni ya kutoa huduma za utalii na wenye magari ya utalii. 

 WAZIRI Mkuu, akionyesha  cheti hicho. Wengine kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji), Doroth Mwaluko,  Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)  William Kallaghe na  Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Ayoub Ryoba.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dk. Allan Kijazi alisema, Chaneli ya Tanzania Safari imekuja katika wakati muafaka kwa kuwa itaongeza juhudi za taasisi zao kutangaza vivutio vilivyopo nchini na hivyo kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wa nje.

  KASIM  Majaliwa (kushoto) akiteta na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya  Mamlaka ya Usimazi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali Mstaafu, Hamisi Semfuko.


Alisema, uwepo wa chaneli hii utasaidia kuondoa upotoshaji wa makusudi uliokuwa ukifanywa na baadhi ya nchi kuwa vivutio fulani viko kwenye maeneo yao wakati siyo kweli.

No comments