WAZIRI MKUU KUWAPOKEA WATALII 300 KUTOKA CHINA.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,
akisalimiana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad Group ya China, Liehui
He, ofisini kwake Jijini Dodoma, jana Januari
19, 2019. (Picha zote na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Na Irene Bwire
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,
ameahidi kupokea kundi la watalii wasiopungua 300 ambao wanatarajiwa kuwasili
nchini Machi, 2019.
Watalii hao ni kundi la kwanza
miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kuwasili nchini katika mwaka huu 2019
chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya
Utalii Tanzania na Kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.
Alitoa ahadi hiyo jana Januari 19,
2019 alipokutana na Mwenyekiti wa Touchroad Group, Liehui He na Mwenyekiti wa
Bodi ya Utalii, Jaji Thomas Mihayo ofisini kwake Mlimwa, Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo
baada ya kuelezwa na He, kwamba kundi
hilo la watalii likiwa Djibouti litapokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo na
likienda Zimbabwe, litapokelewa na Rais wa nchi hiyo.
“Tanzania imeamua kuweka mkakati wa
kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kuboresha miundombinu ya usafiri na kukuza
utalii kupitia vivutio vya vyakula vya asili, mavazi ya asili, wanyama, fukwe
za bahari na milima. Kwa hiyo, ujio wa kundi hili kubwa unatoa fursa mpya ya
kutangaza vivutio vya nchi yetu.
“Nitoe wito kwa Watanzania wanaoishi
maeneo ya jirani na vivutio vyetu, wachangamkie fursa ya ujio wa watalii hawa
katika maeneo mbalimbali.
“Wakifika Dar es Salaam, wanaweza
kwenda Kigoma kuona Ziwa Tanganyika, mbuga zilizoko Nyanda za Juu Kusini,
Arusha au vivutio vya Zanzibar. Tujiandae, tuwe tayari kuwauzia bidhaa
mbalimbali,” alisema.
Pia, alisema amefurahishwa na wazo
lao la kuifanya Dar es Salaam iwe kitovu cha utalii (tourist hub) kwa makundi
ya watalii ambayo yatakuja Tanzania na baadaye kutoka Tanzania kwenda Lusaka,
Harare, Johannesburg na Djibouti.
Mwenyekiti huyo ambaye aliwasili
nchini juzi, ameambatana na ujumbe wa watu 31 ambao unajumuisha waandishi wa
habari, wasanii, wanamuziki na watu mashuhuri.
Akiwa Beijing, China, wakati
akishiriki mkutano wa Jukwaa la Biashara baina ya Tanzania na China
lililofanyika Septemba 2018, Waziri Mkuu alikutana na uongozi wa Kampuni ya
TouchRoad ambayo ilionyesha nia ya kutangaza fursa za utalii zilizopo hapa
nchini.
Ziara ya He, ni sehemu ya
utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa kati ya kampuni ya TouchRoad na Bodi ya
Utalii ya Tanzania, Novemba 2018.
Mapema, He alimweleza Waziri Mkuu nia ya kampuni hiyo kutekeleza
makubaliano yao ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika soko la
China ili kuvutia watalii wapatao 10,000 waitembelee Tanzania katika mwaka
2019.
“Tumepanga kuleta watalii 10,000 kwa
mwaka huu wa 2019 na tumeweka lengo la kuongeza idadi hiyo kwa asilimia 20 kila
mwaka kwa muda wa miaka mitano. Pia tuna lengo la kuitumia ndege ya ATCL ili
ilete watalii moja kwa moja kutoka Shanghai, China,” alisema.
Akielezea ujio wa kundi la kwanza la
watalii He, alisema kundi hilo litakaa Djibouti kwa siku moja, Tanzania siku
nne (tatu za kulala) na Zimbabwe siku tatu (mbili za kulala) na kisha kurejea
China.
Alisema wanapanga kila mwezi wawe na
kundi kubwa la watalii ambao watakuwa wanafikia Tanzania na kupelekwa nchi
nyingine kwa sababu Wachina wengi hupenda kufanya utalii kwa siku walau 10,
lakini wapelekwe maeneo matatu au manne tofauti kuona vivutio vya aina nyingine
badala ya kukaa sehemu moja kwa kipindi chote hicho.
“Watalii hawa wakija kwa siku tatu
au nne, wana uhakika wa kutumia dola za Marekani zaidi 2,000, wakienda eneo
jingine watatumia fedha pia,” alisema.
Alisema, namna hiyo tuna uhakika wa
kuongeza pato la Taifa, lakini pia tuna uhakika wa kutengeneza ajira kwa Watanzania.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa (kulia),
akizungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad Group ya China, Liehui
He, ofisini kwake Jijini Dodoma.
No comments