Breaking News

MAKAMU WA RAIS AZITAKA HALMASHAURI KUTOA 10% KWA VIJANA, AKINA MAMA NA WALEMAVU.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatoa asilimia 10% ya mapato yake kwa Wanawake, Vijana na Walemavu kwa mujibu wa sheria.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi katika Viwanja vya TASAF wilaya ya Sikonge mkoani Tabora ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo.

“Niagize Halmashauri zote kuhakikisha zinatoa fedha hizo kama ilivyopangwa bila riba yeyote kwani fedha hizi zipo kisheria na kwa kutozitoa ni kuvunja sheria”alisema Makamu wa Rais.

Aidha, amesisitiza Halmashauri kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha fedha zinazokopeswa kwa vikundi zinarejeshwa kwa kuwa lengo la fedha hizo ni kuwanufaishwa walengwa zaidi huku akishauri kuwepo na makundi yenye mradi unaoleta tija kwa manufaa ya wengi.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kutoharibu mazingira kwa kukata miti kwani hasara ya kukata mti ni kubwa kulikoni faida wanayoipata hivyo amewashauri kutumia teknolojia mpya ya Solar na Umeme kama ilivyoshauriwa na wataalamu.

Wakati huohuo Mbunge wa Jimbo la Sikonge ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda amesema mpaka 2021 kwa mara ya kwanza vijiji vyote wilayani Sikonge vitapata umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Kakunda ameleeza namna wananchi wa Jimbo lake walivyoridhishwa na kasi ya maendeleo ambapo Serikali imetoa pesa katika miradi ya afya, miradi ya elimu na kuboresha miundombinu ya barabara.

Kwa upande mwingine Waziri wa Madini Doto Biteko amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kurudisha uchumi wa madini kwa Watanzania.

No comments