Breaking News

RAIS MAGUFULI AANDALIWA MKESHA MKUBWA NCHINI.ASKOFU wa Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches (TFC), Godfrey Mallasy amesema  Mkesha Mkubwa wa Kitaifa ambao hufanyika tarehe 31 Desemba kila mwaka kwa ajili ya kuliombea Taifa, mwaka huu utafanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma hivyo utatumika kwa mapokezi ya Rais John Magufuli Jijii humo.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Februari 11, 2019) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kanisa la Dodoma Christian Centre mara baada ya kumaliza ibada maalumu ya kuombea ujio wa Rais Magufuli jijini Dodoma.
  
“Ndoto ya Serikali kuhamia Dodoma inakaribia kutimia kwa sababu wizara zote zimeshahamia hapa na Mheshimiwa Rais wetu anakaribia kuhamia. Kwa hiyo, viongozi wa kiroho tunao wajibu wa kumuandalia makazi yake ya kiroho. Jambo lolote likitokea, basi ujue limeanzia rohoni,” alisema.
  
“Rais wetu anakuja hapa na ana ndoto kubwa, je ndoto hizo zitaenda wapi? Jeshi la Mungu liko hapa, kwa hiyo ndoto hizo hazitadidimia kama jina lilivyo. Kupitia kuangusha ngome na madhababu za Dodoma, mambo yanaenda kubadilika,” alisisitiza.

Alisema maombi hayo yamefanyika ili Rais Magufuli aweze kutawala kwa amani na kutekeleza ndoto zake za kuijenga Tanzania mpya kwa mafanikio makubwa. Alisisitiza Watanzania wote, kuanzia kwenye ngazi ya familia, waendelee kuliombea Taifa liwe na amani kwa sababu pasipokuwa na amani, hakuna kinachoweza kufanyika.

Aidha katika ibada hiyo, Askofu Mallasy aliwaongoza wachungaji wengine 20 wa TFC kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na wachungaji kutoka makanisa ya FPCT, EAGT, TAG, KKKT na Anglikana kuimba wimbo wa Taifa na kufanya kitendo cha kumpokea Rais Magufuli.

Mkesha wa kuliombea Taifa, umekuwa ukifanyika nchini kila mwaka kuanzia mwaka 1997.

No comments