Breaking News

WANAOKWAMISHA RUFAA ZA WATUMISHI KUKIONA CHA MTEMA KUNI.

Imeeleza kuwa, baadhi ya waajiri na watumishi wa umma wamekuwa wakikaidi au kuchelewa kutekeleza maelekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma ya kuwataka kuwasilisha vielelezo vinavyowezesha ushughulikiaji wa rufaa za mashauri ya watumishi jambo linalokwamisha ushughulikiaji wa rufaa za watumishi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alipokuwa akizungumza na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma Jijini Dar es Salaam.
Amewataka Watendaji katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Mamlaka, Sekretarieti za mikoa na Halmashauri za wilaya nchini  kutokwamisha jitihada za Tume ya Utumishi wa Umma katika kushughulikia rufaa za mashauri ya watumishi wa umma kwa kutuma vielelezo sahihi vinavyohitajika.
Pia Mkuchika amewataka waajiri na watumishi wa umma nchini kutoa ushirikiano wa dhati kwa Tume ya Utumishi wa Umma kila wanapotakiwa kufanya hivyo na kumwagiza Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma kuorodhesha waajiri wote watakaoendelea kukaidi maagizo ya Tume ili hatua za kinidhamu zichukuliwe.
Aidha amewatahadharisha watumishi na waajiri wanaokwamisha michakato ya ushughulikiaji wa rufaa za watumishi kuwa wanaathiri dhana nzima ya utawala bora na wanakwamisha utoaji wa haki kwa watumishi wa umma na kusisitiza kuwa hatomvumilia mwajiri au mtumishi yeyote anayeharibu heshima yake aliyoijenga kwa miaka mingi.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma, Naibu Katibu, Tume ya Utumishi wa Umma Rosy Elipenda amemhakikishia Waziri Mkuchika kuyafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa na kuongeza kuwa Tume itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu bila upendeleo wowote.

No comments