Breaking News

TAA WAJIDHATITI NA UENDESHAJI WA JENGO LA TATU LA ABIRIA


MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imebainisha kwamba itakua tayari kwa ajili ya utoaji wa huduma za uendeshaji katika Jengo la tatu la abiria pale mradi wa Ujenzi utakapokuwa umekamilika.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha alipokua akitoa taarifa fupi ya TAA kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Miundombinu ilipofanya ziara katika eneo la Ujenzi huo.

Rwegasha amesema hatua mbalimbali za Maandalizi tayari zimeshachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wa huduma hizo, ikiwa ni pamoja na utoaji wa mafunzo yanayohitajika kwa watendaji wa ngazi mbalimbali.

“Mamlaka  inaendelea kufanya taratibu za maandalizi ya utoaji huduma za uendeshaji katika Jengo la tatu la abiria, katika mpango huo tayari mafunzo kwa watendaji mbalimbali yameanza na hivi sasa watendaji 40 wapo Korea ya kusini katika mafunzo” amesema Bw. Rwegasha.

Aidha Rwegasha amebainisha kwamba katika utekelezaji mpango wa uhamishaji shughuli, Mamlaka imejipanga kuhakikisha hakuna madhara yeyote ya kiuendeshaji yanajitokeza.

“Mamlaka itahakikisha kwamba inazuia athari zote zinazoweza kutokana na zoezi la uhamishaji wa shughuli za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa Ndege na abiria, uharibifu wa mitambo,madhara ya kiusalama na kadhalika.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Idara ya Viwanja vya Ndege katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Emmanuel Raphael  amebainisha kwamba hadi kufika mwezi February 2019 utekelezaji wa kazi zote ulifikia asilimia 95.

“Ujenzi wa kazi zote za Ujenzi umefikia 95%, ambapo mchanganuo unaonesha kwamba ujenzi wa jengo umefikia 96%, maegesho ya magari 92%, maegesho ya ndege 98% na kwa ujumla kazi zinaenda vizuri na zinatarajiwa kukamilika Mei 31, 2019”, alisema Mhandisi Raphael.

Naye, Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amebainisha kwamba mpaka sasa Wananchi wa Kipawa waliopisha upanuzi wa Kiwanja wameshalipwa fidia na kwamba mpaka sasa hamna mgogoro wa fidia.

Akitoa majumuisho baada ya ziara ya kamati katika eneo la ujenzi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Seleman Kakoso amesema kwa ujumla Kamati imeridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kwamba wameridhishwa na namna pesa ya serikali ilivyotumika.

“Kwa ujumla Kamati imeridhishwa na hatua ya Ujenzi iliyofikiwa, matumizi ya pesa ya Serikali yanaonekana ni mazuri, lakini natoa wito kwa TAA kuongeza kasi ya maandalizi ili kwenda sawa na kasi ya ujezi huu, lakini pia mjipange kuongeza wafanyakazi ili kuhakikisha kwamba watendaji wa huduma za uendeshaji wanajitosheleza”, amesema  Kakoso.

No comments