Breaking News

BODI MPYA YA TAASISI YA UTAFITI WA MIFUGO (TALIRI) YAKABIDHIWA MAJUKUMU.


 
SERIKALI imeitaka bodi mpya ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) kufanya tafiti za kitaifa ili kuondoka dhana ya taasisi nyingine ambazo zimejikita kufanya tafiti za kibinafsi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga  Mpina amesema hayo wakati wa kuzindua Bodi hiyo Jijini Dodoma yenye Wajumbe nane  ambapo Rais Dkt. John Magufuli alimteua Mwenyekiti wa Bodi ya TALIRI na Waziri akateua Wajumbe saba (7) wa Bodi hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Waziri Mpina alisema Bodi inatakiwa kufanya mabadiliko katika shughuli za Utafiti ili Sekta ya mifugo ipate mafanikio zaidi.

“Tumeteua wajumbe hawa kutokana na uweledi na uzoefu wao mkubwa katika maeneo mbalimbali ambayo wamewahi kutumikia, kwa hiyo tunategemea watafanya kazi kwa bidii ili kuleta matokeo chanya,” alisema Mpina. 

“Naomba mjikite kwenye Utafiti wa Kitaifa tunahitaji kupata matokeo chanya," alisisitiza Waziri Mpina.

Aidha,  amesema Taasisi nyingi za Utafiti hapa nchini zimejikita kufanya Tafiti za wageni, na kuacha jukumu la kufanya Tafiti za migogoro ya Wakulima na wafugaji.

Vilevile Waziri Mpina amesema timu inayotangazwa ina jukumu kubwa la msingi la kusimamia Tafiti za nchi ambazo ni kitovu cha shughuli za mifugo. 

“Kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha na taasisi hii ya TALIRI Namba 4 ya mwaka 2012 imeainisha majukumu ya bodi ya kamati hii kuanzia kifungu cha 8 hadi 11 ambayo yanatakiwa kutekelezwa na bodi hii,” alieleza Mpina.

Amesema pia, Tanzania ni ya pili kwa Afrika kuwa na mifugo mingi lakini uzalishaji wa mazao ya mifugo ni mdogo, wakati kuna ardhi nzuri na maji ya kutosha jambo ambalo halileti picha nzuri.

Alifafanua zaidi kuwa, “Malisho mazuri yapo kwetu kwa nini tushindwe uzalishaji na nchi jirani, Tanzania tuna zaidi ya ng’ombe milioni 30.5, mbuzi milioni 18.8 na kondoo milioni 5.3, katika nchi ambayo ina mifugo na wafugaji.”

“Tunahitaji Bodi hii ya Utafiti iliyopewa dhamana katika shughuli za utafiti ifanye mnyororo mzima kuanzia uzalishaji na mazao yake yanayozalishwa.” Alisema Waziri Mpina

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji Mahmoud Mgimwa alisema, wao kama Wabunge watasimamia na kuishauri serikali na kuwekeza vya kutosha kwenye eneo la Utafiti. 

“Tutahakikisha TALIRI inapata fungu la kutosha ili kuhakikisha inaendelea na inasonga mbele.” alisema Mhe. Mgimwa.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kwa niaba ya Katibu Mkuu anayeshughulikia Mifugo Dkt. Angello Mwilawa alisema, Bodi hiyo iko kikazi na itahakikishia italeta matokeo chanya katika tafiti zake. 

Dkt. Mwilawa alisema , wanafurahi kuzinduliwa kwa bodi hiyo huku akisema watashirikiana na Wizara ya Migugo na Uvuvi katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na wanasonga mbele. 

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Sebastian Chenyembuga alisema, kuteuliwa kwa bodi hiyo kutaleta manufaa makubwa kwa mwananchi na kuhakikisha kuwa wawanatekeleza majukumu yao ipasavyo.

No comments