Breaking News

UVCCM YAAHIDI NEEMA KWA WENYE MAHITAJI MAALUM.


Na EZEKIEL NASHON, KONGWA.

MBUNGE wa viti maalumu anayewakilisha kundi la vijana Mariam Ditopile, ameahidi kuwachimbia kisima cha maji, shule ya msingi Mkoka, ya  watoto wenye mahitaji maalumu, chenye thamani ya shilingi milioni kumi na tano(15,000,000) lengo ni kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika shule hiyo.

Amefikia uamuzi huo wakati wa ziara ya kamati ya utekelezaji ya UVCCM, walipotembelea shule hiyo iliyopo kata ya Mkoka Wilayani Kongwa, na kupokea taarifa kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Paulo Mgolofu, kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya maji.

Mgolofu ameeleza kuwa kwa sasa wanayanunua mitaani na kuyahifadhi katika tanki dogo, na mara nyingi hupata changamoto kutokana na kutopatikana maji kwa wakati na kuleta usumbufu kwa watoto hao wenye ulemavu mbalimbali.

“Kwa kweli mgeni rasmi tatizo la maji hapa limekuwa kubwa sana, ukiangalia watoto hawa ni walemavu, hivyo maji ni muhimu sana kwao ila upatikanaji ndio kero kubwa”, amesema Mwalimu Paulo.

Amesema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi mia moja na sita(106) wa kutwa na bweni, inahudumiwa na serikali, kwa upande wa chakula wamekuwa wakipata kwa wakati, lakini bado kunachangamoto ya mabweni kwani kwa sasa wanabweni moja ambalo wameligawa pande mbili moja watoto wa kike na upande wa kiume.

Pia amesema shule hiyo inaupungufu wa walimu wenye taaluma ya viziwi ambapo imekuwa changamoto katika ufindishaji wa wanafunzi hao, shule pia haina wigo hali inayosababisha watoto hao kuwa katika wakati mgumu.

Licha ya changamoto hizo shule inafanya vizuri kitaaluma ambapo kwa mwaka jana kuna mtoto ambaye mlemavu wa mikono na anatumia miguu kuandika lakini alipata A ya hesabu.

Mariam Ditopile ameahidi kuchimba kisima cha maji na kutoa mbuzi mmoja na vinywaji kwa ajiri ya watoto katika sikuku.

“Ni seme kweli nimeguswa sana na jambo hili, mimi binafsi nitajitolea kuchimba kisima hapa shuleni angalau hawa watoto waweze kupata huduma ya maji,nitajitahidi nianze haraka sana ili watoto hawa wapate maji ya uhakika” amesema Mariam.

Aidha amewataka walimu kujitoa kwa moyo katika kuwa saidia watoto hao bila ya kuchoka, ili angalau nao wafikie ndoto zao katika elimu, shule hiyo ina wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la sita kwa sasa.

No comments