Breaking News

RAIS MAGUFULI AWAITA WANAMIBIA KUWEKEZA TANZANIA.Rais Dkt. John Magufuli amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika na ameikaribisha kampuni ya Meatco ya Namibia kuja kuwekeza nchini Tanzania.

Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 28 Mei, 2019 alipotembelea kiwanda cha nyama cha kampuni ya Meatco kilichopo Jijini Windhoek Namibia wakati wa Ziara yake ya kikazi nchini humo.

Rais Magufuli ameelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho Jannie Breytenbach kuwa kiwanda kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 630 kwa siku, kimeajiri wafanyakazi 650 na kwamba kampuni hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuanzisha viwanda vya nyama.

Kabla ya kutembelea kiwanda hicho Rais Magufuli alitembelea na kuweka shada la maua katika eneo la mashujaa (Heros Acre) waliopigania ukombozi wa Namibia, lililopo nje kidogo ya Jiji la Windhoek nchini humo.

Katika eneo hilo wamezikwa mashujaa wa ukombozi wa Namibia ambao baadhi yao walipata mafunzo katika kambi ya Kongwa nchini Tanzania, wengine walikuwa maafisa wa Chama cha SWAPO ambao ofisi zao zilikuwa Jijini Dar es Salaam na wengine ni viongozi wakuu walioendesha mapambano wakiwa nchini Namibia.

Baadhi ya mashujaa waliozikwa katika eneo hilo ni Ndimo Hamaambo, Peter Nanyemba, Theo-Ben Gurirabo na Toivo ya Toive.

Rais Magufuli ameongozana na mwenyeji wake Rais Hage Geingob.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli ameongozana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Waziri wa Kilimo  Japhet Hasunga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi.

Kabla ya kuondoka nchini Namibia kwenda nchini Zimbabwe ambako anakwenda kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Pili wa Namibia  Hifikepunye Pohamba Jijini Windhoek.


No comments