Breaking News

RAIS MAGUFULI AWASILI ZIMBABWE KWA ZIARA YA KITAIFA YA SIKU 2.


Rais Dkt. John Magufuli leo tarehe 28 Mei, 2019 amewasili katika Jiji la Harare nchini Zimbabwe ambapo anafanya Ziara Rasmi ya Kitaifa ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Robert Mugabe, Rais Magufuli amepokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais Mnangagwa kisha kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na kupigiwa mizinga 21.

Baadaye leo, Rais Magufuli atakuwa na mazungumzo ya falagha na mwenyeji wake, Rais Mnangagwa na kisha atahudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Rais Mnangagwa kwa heshima yake.

Kesho, Rais Magufuli atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake na kisha atatembelea na kuweka shada la maua katika eneo la mashujaa wa ukombozi wa Zimbabwe.

Katika ziara hii Rais Magufuli ameongozana na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Philip Mangula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga.No comments