Breaking News

WANANCHI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KUFANIKISHA KATAZO LA MIFUKO YA PLASTIKI.


MKUU wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori, amewataka Wananchi wa Wilaya hiyo kushirikiana na Serikali kufanikisha mpango wa kusitisha matumizi ya mifuko ya plastiki na kutumia mifuko mbadala kwaajili ya kujikinga na madhara ya kiafya na kukuza maendeleo ya uchumi wa Taifa na mtu mmojammoja.

Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya wiki ya usafi wa mazingira zilizofanyika kwenye viwanja vya Manzese Makori ametaja hatua zilizochukuliwa na wilaya yake ikiwemo ni pamoja na kutenga maeneo ya kusalimisha mifuko hiyo pamoja na kufanya maonyesho mbalimbali kwaajili ya kutoa elimu juu ya matumizi ya mifuko mbadala na usafi wa mazingira.

“Pamoja na kuwa na nguvu ya kisheria swala hili linahitaji ushirikiano toka kwa wananchi na uhamasishaji, wananchi waache kuagiza, kusambaza na kuuza lakini pia wasalimishe mifuko hiyo katika ofisi zetu za kata, pia wenye shehena wapeleke maeneo ya simu 2000.” Amesisitiza makori.

Kuhusu ugonjwa wa dengue Makori amesema kama serikali wameanza kupuliza dawa katika kaya mbalimbali kwenye kata zote nne lakini amewataka wananchi kusafisha mazingira kaajili ya kuteketeza mazalia ya mbu yanayosababisha ugonjwa huo.

“Pia kuna taarifa za ugonjwa wa kipindupindu ndani ya Mkoa wetu na mvua bado zinanyesha hivyo niwatake wananchi wote kuzingatia usafi katika maeneo yao ili kuepuka magonjwa hayo ya mlipuko.” Amesema Makori.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wilaya ya ubungo Betrece Dominick amewatoa  hofu na kuwataka wananchi kutii sheria na kuacha kutupa mifuko hiyo katika maeneo rasmi ya kutupa taka badala yake wakaisalimishe katika maeneo waliyo elekezwa ambapo ni kwenye ofisi za kata.

Kilele cha maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Tumia mifuko mbadala kwa ustawi wa afya ya mazingira na maendeleo ya uchumi itakuwa ni jumatano june 5, 2019.

No comments