Breaking News

BETHEL MISSION SCHOOL WAANDAA SEMINA KAMAMBE KWA WAJASRIAMALI

Na Bashir Nkoromo
Bethel Mission School iliyopo Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, imeandaa Kongamano la siku tano kwa Wajasiriamali ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia wanajamii wanaoizunguka shule, kwa kutambua kuwa  wao ni sehemu ya mafanikio ya shule hiyo.

Mkurugenzi wa Shule hiyo Emmanuel Mshana alisema jana kwamba Kongamano ambalo litawahushisha pia wafanyakazi wa shule hiyo, litaanza Jumatatu Juni 10 hadi Ijumaa Juni 14, 2019 katika Viwanja vya Bethel Missioni School, eneo la Ubungo Makuburi na kwamba hakuna gharama zozote watakazotozwa washiriki.

"Shule yetu ni ya Missioni ipo chini ya Kanisa la Wasabato wa Matengenezo, inaendesha Nursary na Primary na ni ya mda mrefu sana, kwa ukweli shule hii imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma na tunaamini mafanikio haya yamechangiwa pia na jamii inayotuzunguka.

Sasa tumeona ni vema tuweze kuisaidia jamii hii pamoja na Wafanyakazi wetu kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali, kwa hiyo shule imeamua kudhamini Programu ya Ujasiriamali, itakayochukua siku tano, kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, Juni 14, 2019. Programu hii ni bure, nasema ni bure kabisa hakuna gharama yoyote ya kiingilio", Alisema Mshana.

Alisema, mafunzo kwenye Program yatatolewa na Mchungaji Ezrael Ngatunga ambaye Mshana anamwelezea kuwa ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya ujasiriamali na kwamba jumla ya masomo 14 yatatolewa kwa Washiriki ikiwemo kilimo cha uyoga ambacho alisema ni kilimo rahisi lakini chenye manufaa makubwa ambacho mtu anaweza kukifanya hata ndani ya chumba kimoja.

"Wasiriki watafundishwa jumla ya masomo 14, ikiwemo kilimo cha uyoga, kutengeneza sabuni za kunawia, kutengeneza ubuyu wa rangi, sabuni za kuogea hizi za miche, watajifunza pia  kutengeneza sababu za magadi ambazo zinaitwa sabuni za Kigoma, watajifunza kutengeneza vikoi vya mwendokasi, Batiki na utaalam mwingine mbalimbali ikiwemo kutotolesha mayai kwa kutumia maboksi", alisema Mshana.

Akieleza faida za kilimo cha uyoga, Mchungaji Ngatunga alisema, ni kilimo cha Kidigitali, na kwamba hadi sasa bei ya kilo moja ya uyoga inafikia sh. 20,000 na kilimo ambacho unaweza kuvuna hapohapo chumbani kwa muda mrefu.

No comments