Breaking News

JPM AWAAPISHA WAZIRI, RAS, KAMISHNA MKUU WA TRA NA, ASHUHUDIA SERIKALI IKIPOKEA FEDHA KUTOKA AIRTEL TANZANIA.


Rais Dkt. John Magufuli leo tarehe 10 Juni, 2019 amemuapisha Waziri wa Viwanda na Biashara  Innocent Bashungwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Charles Kichere na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin  Mhede.

Viongozi hao wameapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na hafla ya kuapishwa kwao imehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Paul Makonda.

Katika hafla hiyo Rais Magufuli pia ameshuhudia Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akipokea mchango binafsi wa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1 na Milioni 270 kutoka kwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Bharti Airtel International Sunil Bharti Mittal na shilingi Bilioni 3 (ikiwa ni malipo ya shilingi Bilioni 1 kila mwezi) kutoka Bharti Airtel International, fedha ambazo ni matokeo ya majadiliano kati ya Serikali na kampuni hiyo juu ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio yaliyofikiwa katika mazungumzo kati ya Bharti Airtel International na Serikali ambapo pamoja na kutoa shilingi Bilioni 3 ambazo ni malipo ya miezi mitatu (Aprili, Mei na Juni 2019) kampuni hiyo itaendelea kuilipa Serikali ya Tanzania shilingi Bilioni 1 kila mwezi kwa muda wa miaka mitano ambayo ni sawa na shilingi Bilioni 60.

Rais Magufuli amesema japo kuwa hatua ya kupigania hisa za Serikali na maslahi ya Taifa katika umiliki wa Airtel Tanzania zilibezwa na baadhi ya watu lakini leo nchi inakwenda kunufaika kwa kiasi hicho kikubwa cha fedha ambacho endapo kikielekezwa kujenga Vituo vya Afya, Watanzania watapata vituo 150 kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa wakiwemo watoto, wanawake na wazee.

Ameongeza kuwa majadiliano na kampuni hiyo yameiwezesha Tanzania kuongeza hisa zake katika umiliki wa Airtel Tanzania ambapo zimepanda kutoka asilimia 40 hadi 49, kufutwa kwa deni la shilingi Bilioni 930 ambalo Tanzania ilikuwa inapaswa kulipa kiasi cha shilingi Bilioni 459.13, kubadili muundo wa bodi na menejimenti ya Airtel Tanzania ambapo Mwenyekiti wa Bodi na Mkuu wa Ufundi sasa watateuliwa na Serikali ya Tanzania, Serikali kupata gawio kutokana na faida ghafi kwa hesabu za mwaka 2019 na kutetea maslahi mengine mapana ya Serikali katika kampuni hiyo.

Rais Magufuli amempongeza Sunil Bharti Mittal kwa moyo wake wa kuridhia makubaliano na kukubali kuendelea kufanya kazi kwa maslahi ya pande zote mbili na amebainisha kuwa hatua zilizochukuliwa kwa Airtel Tanzania hazina lengo la kuwafukuza wawekezaji bali kusimamia haki ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Sunil Mittal amempongeza Rais Magufuli kwa hatua anazochukua kupigania maslahi ya Watanzania na ameeleza kuwa anaamini baada ya makubaliano yaliyofikiwa Airtel Tanzania itazidi kukua na kuungwa mkono na Watanzania wengi kwa kuwa nao wanamiliki nusu ya hisa zake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi aliyeongoza Kamati ya Majadiliano kwa niaba ya Serikali na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wamempongeza Rais Magufuli kwa kutia msukumo mkubwa katika kufanikisha majadiliano hayo na kwamba fedha hizo ambazo zimeelekezwa katika ujenzi wa Hospitali ya Uhuru Mkoani Dodoma zitaacha kumbukumbu muhimu ya dhamira ya dhati ya Rais Magufuli kuwapigania Watanzania.

Kwa viongozi walioapishwa, Rais Magufuli amewataka kwenda kuchapa kazi, na ameweka wazi kuwa hutengua uteuzi na kuteua viongozi kwa kuwa anataka viongozi wanaofanya kazi ya kutimiza matarajio ya Watanzania na kwamba hatua hiyo haimaanishi anamchukia mtu yeyote.

Amemtaka Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Mhede kuhakikisha anashughulikia changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo zikiwemo kuongeza ukusanyaji wa mapato unaovuka shilingi Trilioni 1.3 zilizofikiwa tangu Dkt. Philip Mpango akiwa Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA mwaka 2015 na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa TRA ambao wamekuwa wakiharibu sura ya mamlaka hiyo kwa vitendo vya rushwa, kuwanyanyasa walipa kodi na kutokusanya kodi ipasavyo.

Kwa Bashungwa, Rais Magufuli amemtaka kushughulikia dosari zilizopo katika Wizara ya Viwanda na Biashara zikiwemo kushughulikia kero za wafanyabiashara kwa wakati, kusimamia vizuri taasisi zilizopo katika wizara hiyo, kushughulikia tatizo la masoko ya mazao likiwemo zao la korosho na kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi.

Rais Magufuli amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Kichere kwenda kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Njombe katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika Mkoa huo.

No comments