Breaking News

MAAGIZO YA RAIS MAGUFULI KWA BAADHI YA WATEULE WAKE.Rais  Dkt. John Magufuli leo tarehe 04 Juni, 2019 amekutana na Makatibu Tawala wa Wilaya zote na Maafisa Tarafa wa Tarafa zote hapa nchini, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kujiamini, kuzingatia sheria na taratibu na kusimamia kwa karibu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ya kazi.

Rais Magufuli amewaagiza Maafisa Tarafa hao kujenga utaratibu wa kuwatembelea, kuwasikiliza na kutatua kero na migogoro mbalimbali inayowakabili wananchi pamoja na kuchukua hatua pale ambao mambo hayaendi sawa ikiwemo utekelezaji mbaya wa miradi kama vile ujenzi wa majengo ya Serikali, barabara, miradi ya maji na mingine.

Amewataka Makatibu Tawala kutambua nafasi walizonazo Maafisa Tarafa na wote kufanya kazi kwa ushirikiano badala ya Maafisa Tarafa kugeuzwa kuwa wasaidizi wa Makatibu Tawala wa Wilaya ili majukumu ya Serikali yaliyopo katika maeneo hayo yatekelezwe kwa mafanikio na ufanisi mkubwa.

Rais Magufuli ameongeza kuwa hatarajii kuona Afisa Tarafa anajihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili na utovu wa nidhamu au hafuatilia utekelezaji wa miradi mikubwa iliyopo ama inayopita katika eneo lake kwa kuwa kufanya hivyo kutakuwa kunadhihirisha kuwa haimudu kazi hiyo.

Aidha, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kutambua mipaka ya kazi yao, kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato, kusimamia kwa ukaribu utoaji wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo, kuhamasisha watu kufanya kazi za uzalishaji mali, kusimamia ulinzi na usalama,kukomesha wizi na ufisadi wa mali za umma na kuyatangaza mafanikio ya Serikali yao ili kuwapa matumaini wananchi.

Kabla ya kuzungumza na viongozi hao, Rais Magufuli amesikiliza maoni na changamoto mbalimbali kutoka kwa viongozi hao ambapo ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya kuwanunulia pikipiki Maafisa Tarafa 399 ambao hawajapata mgao wa pikipiki na pia amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu wa Utumishi na Utawala Bora kuondoa sharti la kutopandishwa cheo kwa Afisa Tarafa ambaye hajapatiwa mafunzo mafupi ya utumishi.

“Maafisa Tarafa wenye pikipiki ni 171 na wasio na pikipiki ni 399, kwa hiyo nimeamua kutoa maelekezo zinunuliwe pikipiki kwa wote ambao hawana pikipiki, lakini nawasihi sana mtumie vyombo hivyo kwa uangalifu, isije ikawa ndio chanzo cha kuwapa ulemavu” amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewapongeza Maafisa Tarafa wote wanaofanya kazi vizuri na kwa ushirikiano na watumishi wenzao wa umma waliopo katika maeneo yao, na kufuatia utendaji kazi mzuri wa Mtendaji wa Kata ya Engarenaibor Wilaya ya LongidoMkoani Arusha Thomas Ngobei, ameagiza apandishwe cheo na kuwa Afisa Tarafa.

Wakitoa maoni na changamoto zao, Maafisa Tarafa hao wamempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwahudumia wananchi na wamemhakikishia kuwa wapo tayari kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kusimamia kwa ukaribu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Waziri wa Utumishi na Utawala Bora George Mkuchika, Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo na Katibu Mkuu wa Utumishi Dkt. Laurian Ndumbaro wamempongeza Rais Magufuli kwa kuandika historia ya kuwa Rais wa kwanza kukutana na Maafisa Tarafa wa nchi nzima na wamewataka Maafisa Tarafa hao kufanya kazi kwa kuzingatia miiko yao ya utumishi, kuleta tija na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Viongozi Wakuu.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa wamewataka Maafisa Tarafa hao kujenga mahusiano mazuri na watumishi wengine wa umma, kutoa taarifa ya yanayotokea katika maeneo yao na kufanya kazi kwa kutanguliza uzalendo na mshikamano wa Taifa.No comments