Breaking News

RAIS MAGUFULI AMPONGEZA RAIS TSHISEKEDI KWA KUCHAGULIWA NA KULETA AMANI DRC.

Rais Dkt. John Magufuli amempongeza Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC),  Felix  Tshisekedi kwa juhudi zake za kutafuta amani nchini mwake baada ya kuingia madarakani katika uchaguzi wa kidemokrasia na kubadilishana madaraka kwa amani uliofanyika kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo tarehe 13 Juni, 2019 wakati akitoa hotuba katika Dhifa ya Kitaifa aliyoiandaa kwa heshima ya Rais Tshisekedi ambaye amewasili hapa nchini leo kwa Ziara ya Kitaifa ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais Magufuli.

Rais Magufuli amempongeza, Rais Tshisekedi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa DRC katika uchaguzi wa kihistoria uliofanyika Januari 2019 na kwa juhudi zake za kuunganisha makundi yaliyokuwa yakipingana nchini DRC. Amemhakikishia kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi hizo.

“Pamoja na kukupongeza wewe Rais Tshisekedi pia nampongeza Rais Mstaafu wa DRC Joseph Kabila kwa kufanikisha mchakato wa kubadilishana madaraka kwa amani” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema kwa kutambua umuhimu wa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo, Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi wengi wanaotokana na machafuko kutoka nchini DRC na amemhakikishia kuwa Tanzania itadumisha udugu, urafiki na ujirani mwema na nchi hiyo.

Pia amesisitiza kuwa Tanzania haitowaondoa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaoshiriki katika operesheni ya ulinzi wa amani mpaka hapo hali ya amani itakapotengemaa.

Kwa upande wake Rais Tshisekedi amemshukuru Rais Magufuli na Watanzania wote kwa kuendelea kuwa majirani wema na ndugu wa kweli wa DRC na amemhakikishia kuwa Serikali yake itaimarisha uhusiano huo ikiwemo kutilia mkazo maombi ya nchi hiyo kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tshisekedi amebainisha kuwa baada ya kuimarisha amani nchini DRC, Serikali yake sasa inaelekeza jitihada katika kuimarisha usalama nchini humo na ameishukuru Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika ulinzi wa amani ya DRC.

“Ziara hii ni ishara ya kuonesha kuwa DRC inatambua umuhimu wa uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania, na sisi DRC tumejipanga kuhakikisha uhusiano huu tunaukuza zaidi” amesema Rais Tshisekedi.

Ameongeza kuwa nchi za Afrika zinayo changamoto ya kuimarisha utengamano wake wa kiuchumi, na kwa maana hiyo anaona umuhimu mkubwa wa kutumia fursa mbalimbali zilizopo likiwemo Ziwa Tanganyika katika kukuza biashara na pia kuimarisha miundombinu ya barabara, nishati na kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kuleta matokeo makubwa katika siku za mbeleni.

Dhifa ya Kitaifa iliyofanyika leo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Ngoyai Lowassa, Mawaziri, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wabunge, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa na wafanyabiashara.

Rais Tshisekedi kesho asubuhi atatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumiwa kupitisha mizigo ya DRC na baadaye atafanya mazungumzo rasmi na mwenyekiti wake Mhe. Rais Magufuli kabla ya kurejea nchini DRC.

No comments