Breaking News

SERIKALI INAJENGA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU KUWAWEZESHA WATUMISHI WAKE KUPATA MAKAZI BORA.SERIKALI imeendelea kuwajali Watumishi wa Umma nchini kwa kuwajengea nyumba bora za gharama nafuu kupitia miradi ya ujenzi wa nyumba inayotekelezwa na Watumishi Housing Company katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha watumishi kumiliki nyumba bora za kuishi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa  alipotembelea miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi Gezaulole Kigamboni na Bunju B mkoani Dar es Salaam.

Dkt. Mwanjelwa amesema, amejionea nyumba zilizojengwa kisasa, gharama nafuu na zenye viwango vinavyostahili kwa makazi ya watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambao ndio walengwa wakuu wa miradi hiyo.

Aidha, amewaagiza watendaji wa Watumishi Housing Company kuhakikisha wanakuwa na mkakati madhubuti wa kutoa taarifa kwa watumishi wa umma juu ya uwepo wa nyumba zilizojengwa na kampuni hiyo, sehemu zilipo na bei elekezi kwa wanaohitaji kununua, ikiwa ni pamoja na bei ya kupangisha.  

Amekamilisha ziara yake ya kikazi mkoani Dar es Salaam ya kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Watumishi wa Umma na  wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji wa Watumishi Housing Company.


No comments