Breaking News

SIKU YA UTUMISHI WA UMMA BARANI AFRIKA KWA MWAKA 2019 KUFANYIKA TANZANIA.
Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inaratibu maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika kwa mwaka 2019 ambayo hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema maadhimisho hayo kwa mwaka huu, yanatarajiwa kufanyika Nairobi, Kenya kuanzia tarehe 21 hadi 23 Juni, 2019.

Mkuchika amefafanua kuwa, malengo ya kuadhimisha siku hii kila baada ya miaka miwili, ni kuziwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya Usimamizi wa Utumishi na Utawala hususan mafanikio na changamoto ili kuzitumia kama chachu ya kuboresha utoaji huduma kwa umma.

Mkuchika amesema, taasisi zitakazoshiriki katika maadhimisho hayo, ni zile ambazo huduma zake zinalenga moja kwa moja kaulimbiu ya mwaka huu  inayosema “Uhusiano kati ya uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa masuala ya uhamiaji: Kujenga utamaduni wa Utawala Bora, matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika utoaji wa Huduma Jumuishi,” hivyo kuzitaka taasisi hizo kuwa mabalozi wazuri katika kuiwakilisha nchi yetu.

Mkuchika amezitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni pamoja na maonyesho ya kazi za ubunifu zilizofanywa na Taasisi kulingana na Kauli Mbiu, mdahalo kuhusu masuala ya Uwezeshaji wa Vijana, Utawala Bora, matumizi bora ya TEHAMA, Ubunifu katika utoaji Huduma Jumuishi na namna bora ya kujenga maadili katika Utumishi wa Umma.

Mkuchika amesema, katika maadhimisho ya kitaifa, ofisi yake imewaelekeza Watendaji wa Taasisi za Umma, kukutana na watumishi katika maeneo yao ya kazi ili kusikiliza maoni na changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau wa nje kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma wanazozitoa.

Mkuchika ameongeza kuwa, ili kujenga mahusiano mazuri na jamii, Taasisi za Umma zinaweza kuadhimisha wiki hiyo kwa kufanya shughuli za kijamii kama vile za usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali hususan hospitali, sokoni  na katika fukwe za mito na bahari zilizo jirani na maeneo yao ya kazi.

Sanjari na hayo, Mkuchika ameziagiza Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi zote za Umma kuwasilisha taarifa ya namna walivyoshiriki maadhimisho hayo kwa Makatibu Wakuu wa Wizara ambao wataunganisha taarifa hizo na kuziwasilisha kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili Serikali iweze kutumia taarifa hizo kuboresha utendaji kazi.

Aidha, Mkuchika amewapongeza watumishi wote wa umma nchini kwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kuwahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa manufaa na maendeleo ya Taifa letu.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma husherehekewa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kila mwaka kuanzia tarehe 16-23 Juni kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya Nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.

No comments