Breaking News

SERIKALI KUONGEZA NGUVU KUPAMBANA NA RUSHWA NCHINI.Na Ezekiel Nashon, Dodoma.

SERIKALI imesema imeweka nguvu na msisitizo mkubwa katika kupambana na rushwa, kwani rushwa imekuwa ikirudisha sana juhudi za kupambana na umasikini, kujikomboa kiuchumi na kupoteza haki  za watu wengi katika jamii.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma, na naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt Damasi Ndumbaro, wakati akizungumza kwenye kongamano la siku maalumu ya mapambano dhidi rushwa kwa nchi za umoja wa Afrika(AU).

Ambapo umefanyika jijini Dodoma, na kutumia siku hiyo kama ni siku ya kuhamasisha, kuwapa elimu, na kuwajengea uwezo vijana namna ya kupambana na rushwa, ambapo kongamano hilo limehusisha wanafunzi wa vyuo vikuu, na wanafunzi wa sekondari na waandishi wa habari.

Dkt Ndumbaro amesema kama nchi wameweka mkazo mkubwa kuhakikisha wanapambana na rushwa, na kwa kuhakikisha hayo yanafanikiwa Tanzania imejiunga na  kusaini mikataba na itifaki za kupambana na rushwa kimataifa na kikanda.

“Tanzania kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na rushwa imesaini na kuridhia mikataba na itifaki za kupambana na rushwa kimataifa na kikanda, hii ni pamoja na mikataba ya umoja wa kimataifa wa kupambana na rushwa” amesema dkt Ndumbaro.

Ametaja baadhi ya mikataba hiyo ni mkataba wa umoja wa kimataifa wa kupambana na rushwa(UNCAC,2003), itifaki ya nchi za kusini mwa bara la Afrika ya kupambana na rushwa(SADC Protocol Against Corruption, 2001, na mkataba wa mapambano dhidi ya rushwa kwa nchi za afrika(AU Convention on preventing and Combating Corruption, 2003).

Nyingine ni mwanachama wa shirikisho la taasisi za mapambano dhidi ya rushwa barani  Afrika(AAACA) jumuiya ya madola(CAACA) pamoja na Afrika mashariki( EAAACA) amesema Tanzania pia ni mwenyeji wa bodi ya umoja Afrika ya ushauri kuhusu maswala ya rushwa ambapo makao makuu yake yapo Arusha.

Amesema kwa mkazo huo tafiti zinaonyesha kuongezeka kwa kiwango  cha utawala bora kwa kupata asilimia 58.5/100.

“Tanzania imeonekana kuongeza kiwango cha utawala bora kwa kupata alama 58.5/100,na kuwa nchi ya kumi na moja11 kati ya nchi 54 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na 2017 ambapo ilipata alama 57.5/100 na kuwa nchi ya 17 katika bara la Afrika kwa mujibu wa Mo Ibrahim Index of African Governance” amesema.
Aidha amewataka TAKUKURU kuhakikisha wanafanya kazi kwa uwazi na waminifu ili kukomesha vitendo vya  rushwa hapa nchini na kuwa na utawala bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mkuu wa TAKUKURU CP, Diwani Athumani, amesema wao wamekuwa wakifanya kazi na kuhakikisha wanakomesha vitendo vya rushwa hapa nchini.

Amesema wamekuwa wakifanya kazi na kuhakikisha taarifa zinazopatikana zinawafikia wananchi ili waweze kujifunza kuhusu maswala ya rushwa na kuhakikisha mali ambazo hazikupatikana kwa halali zinarudishwa serikalini kwa mujibu wa sheria.

Aidha amesema moja ya changamoto ambazo zinaikabili Taasisi hiyo katika utendaji wa kazi ni pamoja na  kukosekana kwa ushahidi pindi kesi zinapokuwa mahakamani pamoja na ufinyu wa bajeti katika taasisi hiyo.

“Moja  ya changamoto ambazo zinaikabili taasisi hii ni pamoja na mashahidi kushindwa kufika kutoa ushahidi pindi kesi zinapokuwa mahakamani kesi nyingi zinafutwa kutokanna na kukosa ushahidi, pamoja na ufinyu wa bajeti katika kutekeleza majukumu yetu” amesema.

No comments